Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sabiha Gokcen jijini Istanbul umeorodheshwa wa kwanza kati ya viwanja 20 vyenye shughuli nyingi kwa kuzingatia ratiba ya kuondoka kwa wakati, mkuu wa uratibu wa uwanja wa ndege alisema Ijumaa.
Faruk Kacir, mkuu wa uratibu wa uwanja wa ndege HEAS, anasema Sabiha Gokcen imefanikisha kwa asilimia 88 kwa abiria kuondoka kwa wakati, akieleza kulingana na Ripoti ya Kutathmini Utendaji Kazi wa Mashirika ya Ulaya Kwa Usalama wa Safari za Anga (EUROCONTROL).
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal, Kacir anasema uwanja huo wa ndege umepita kiwango cha wastani cha Ulaya cha kuzingatia muda wa safari cha asilimia 72.
Alipongeza mafanikio hayo akieleza ni kutokana na miundombinu ya uwanja wa ndege, uongozaji mzuri wa ndege, na uratibu miongoni mwa wadau pamoja na mkakati wa maendeleo endelevu.
Kacir alisema kuwa uwanja huo wa ndege utapata uwekezaji wa uimarishaji ikiwa ni pamoja na sehemu ya pili ya kupaa na kutua kwa ndege, sehemu ya kuegesha ndege, miradi ya kupanua maeneo na mabadiliko ya kidijitali.
Pia aliwashkuru waongozaji wa safari za ndege, mashirika ya ndege, kampuni za mizigo, wafanyakazi wa uwanja wa ndege na wadau wengine kwa mchango wao wa kusaidia katika mafanikio hayo.
Ukiwa uko upande wa Asia wa Istanbul, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sabiha Gokcen ni moja kati ya maeneo ya Uturuki yenye shughuli nyingi kwa safari za anga, ukiwa na safari za ndani ya nchi na kimataifa.
Mwaka 2025 uwanja huo wa ndege ulihudumia abiria milioni 48.4, ikiwemo milioni 21.2 katika safari za ndani ya nchi na milioni 27.2 kwa safari za kimataifa, kulingana na takwimu za uwanja wa ndege.












