Zaidi ya raia 50 wa Ghana wameuawa katika vita vya Ukraine baada ya “kulaghaiwa kujiunga vitani”, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana amesema baada ya ziara yake jijini Kyiv, Ukraine ambako mazungumzo yalijikuta katika suala la kuajiriwa kwa raia wenye asili ya Kiafrika.
Ripoti kuhusu watu hao kulaghaiwa kwenda Urusi kwa ahadi za ajira na kuishia vitani nchini Ukraine zimeongezeka katika miezi ya karibuni, hali iliyosababisha mvutano kati ya Urusi na baadhi ya nchi husika.
Mamlaka za Urusi zimekanusha kuajiri raia wa Kiafrika kinyume cha sheria kupigana nchini Ukraine.
“Tulipewa taarifa kuwa raia 272 wa Ghana wanaaminika kushawishiwa kujiunga katika vita tangu mwaka 2022, ambapo inakadiriwa 55 wameuawa na wawili wametekwa kama wafungwa wa vita,” Samuel Okudzeto Ablakwa aliandika kwenye ukarasa wa mtandao wa kijamii wa X mwishoni mwa Alhamisi.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, akiwa amesimama pamoja na Ablakwa, alisema zaidi ya Waafrika 1,780 kutoka nchi 36 tofauti “wamjiunga na jeshi la Urusi”.
‘Hivi vita si vyetu’
Ghana, ambayo ina uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na Urusi, inapanga kuongeza kampeni za kuonya raia wake kuhusu mpango wa kuajiri watu kuelekea Urusi kwa ahadi za kazo na kuvunja “mitandao haramu ya kusajili watu kinyume na sheria kupitia mitandao isiyoeleweka ndani ya mamlaka yetu,” Ablakwa aliandika kwenye ukurasa wake wa X.
“Hivi si vita vyetu, na hatuwezi kuruhusu vijana wetu kuwa kinga za binadamu kwa ajili ya wengine,” alisema.
Serikali ya Afrika Kusini imesema wiki hii kuwa raia wake wawili wamefariki dunia wakiwa vitani.
Wawili hao ni tofauti na kundi la raia 17 wa Afrika Kusini waliolaghaiwa kupigana kwa upande wa Urusi nchini Ukraine na ambao wengi wao wamesharejeshwa nyumbani, wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini ilisema katika taarifa.
Kulingana na ripoti ya Idara ya Ujasusi nchini Kenya, zaidi ya Wakenya 1,000 wameajiriwa kupigana kwa upande wa Urusi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imesema Wakenya 27 wameokolewa baada ya kukwama nchini Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema anapanga kutembelea Urusi mwezi Machi kwa mazungumzo kuhusu suala hilo.














