Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amewataka watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kufanya utafiti, ili kupata takwimu sahihi.
“Maofisa Mawasiliano wote jengeni utamaduni wa kufanya tafiti, kupata takwimu sahihi kabla kuzisambaza kwa wananchi na kuhuisha taarifa za kisekta kwenye tovuti,” alisema Mwigulu Nchemba, wakati akifungua mkutano wa 110 wa mwaka wa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia TBC uliofanyika Machi 25, 2026, jijini Arusha.
Waziri Mkuu huyo, aliwataka watayarishaji hao, kutumia vipindi vyao, kutangaza mafanikio ya serikali kusudi wananchi wapate taarifa sahihi.
“Maofisa Mawasiliano wote tumieni kila fursa kutangaza mafanikio ya serikali katika sekta zenu ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi za sekta mnazofanyia kazi,” alisisitiza.
Pia, amewataka watayarishaji hao waandae maudhui yatakayowafikia na kuwagusa vijana kwa lugha wanayoielewa.
“Bila kutumia njia na lugha rafiki kwa vijana, taarifa muhimu zinaweza zisifikie walengwa au kushindwa kuwavutia,” aliongeza.








