Watu wasiopungua 30 wameuawa siku ya Jumatano katika mashambulizi ya magaidi wanaojulikana kama Lakurawa katika eneo la Arewa kwenye jimbo la Kebbi, polisi walisema siku ya Alhamisi.
Msemaji wa polisi Bashir Usman amesema vijiji saba viliharibiwa katika mashambulizi hayo.
Vyanzo viliiambia Anadolu kuwa washambuliaji hao walienda kutoka kijiji kimoja hadi kingine wakifanya mashambulizi, wakilenga raia kwa makusudi.
Sehemu ya jamii ya Mamunu ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya waliouawa 16, vijana watano waliuawa eneo la Awashaka, na wakazi watatu sehemu ya Masama. Jamii zingine zilizoathirika ni Gorin Dena, Kamzo, Dan Mai Rago, na Tungar Bature.
‘Yalikuwa ya kushtukiza’
Wakazi, ambao wengi wao walikimbia katika maeneo ya misitu ya karibu, wanasema hawakutarajia mashambulizi ya kiwango kama hicho. “yalikuwa ya kushtukiza. Walifyatua risasi na kuchoma nyumba,” mwanakijiji mmoja aliiambia Anadolu akitaja asitajwe jina lake.
Kundi la Lakurawa ni la kigaidi linaloendesha mashambulizi yake kaskazini magharibi mwa Nigeria na lina uhusiano na Daesh na ushirikiano na mitandao ya kigaidi ya Mali, Niger, Sokoto na jimbo la Kebbi.
Lakurawa limeibuka kuwa kundi hatari kwa usalama katika miaka ya hivi karibuni, likifanya mashambulizi mabaya kwa jamii za vijijini, kuiba mifugo na kudhibiti kinyume cha sheria baadhi ya maeneo ya kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Machafuko ya hivi karibuni yanakuja huku kukiwa na matatizo ya kiusalama kaskazini magharibi mwa Nigeria, ambapo makundi ya kigaidi yametumia mwanya wa mipaka isiodhibitiwa kushambulia watu, kuiba mifugo na kukabiliana na maafisa wa usalama.





















