Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumanne alizungumzia kuhusu uamuzi wa israel kuitambua Somaliland kama taifa huru na ikiwa nchi pekee iliyofanya hivyo, akisisitiza kuwa uamuzi huo hautofaidi Somalia wala kanda hiyo.
"Ningependa kusisitiza kuwa kwa Israel kutambua Somaliland hakutafaidi Somaliland wala Pembe ya Afrika," Erdogan amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed jijini Addis Ababa.
Uturuki inaamini kuwa nchi katika kanda hii zinatakiwa kutafuta suluhu ya matatizo ya katika kanda yao wenyewe, amesema Erdogan, akitoa wito kwa Pembe ya Afrika kutogeuzwa "kuwa sehemu ya malumbano ya mataifa ya nje.”
Akisisitiza kuhusu ushirikiano kati ya Uturuki na Ethiopia, Erdogan amesema kuwa ni "fahari kubwa" kuwa makampuni zaidi ya 200 ya Uturuki, yenye uwekezaji wa dola bilioni $2.5, yanasaidia kutoa ajira kwa watu karibu 20,000 nchini Ethiopia.
‘Nia ya kufikia bahari’
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa ameiomba Uturuki iwasaidie katika mchakato wao wa kutaka kutumia bahari, akieleza hilo kuwa eneo la msingi watakaloangazia katika mazungumzo yao na rais wa Uturuki.
Abiy alisema katika mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari kuwa alijadili nia ya Ethiopia ya kutaka “kufikia bahari” na kiongozi wa Uturuki na kupongeza majadiliano muhimu na yenye tija kuhusu suala hilo.
Ethiopia, ambayo ni nchi isiyokuwa na bahari tangu uhuru wa Eritrea 1993, imekuwa ikieleza kuwa kufikia bahari kama suala la kipaumbele kimkakati.
Ziara ya Erdogan ni ishara ya ziara ya ngazi ya juu ikiwajumuisha mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Uturuki, miongoni mwa wengine, na imekuja wakati nchi hizo mbili zikitaka kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa hasa wakiadhimisha karne moja ya ushirikiano ulioanza 1926.
Viongozi hao walijadili kupanua ushirikiano wao wa kibiashara,huku maafisa wa Ethiopia wakisema pande zote mbili zinataka kuongeza kiwango cha biashara kisiwe chini ya dola bilioni $1.
Abiy pia alihimiza uwekezaji zaidi wa makampuni ya Uturuki nchini Ethiopia, nchi ambayo tayari ina mkusanyiko mkubwa zaidi wa wafanyabiashara wa Uturuki Kusini mwa jangwa la Sahara, hasa katika sekta ya viwanda na ujenzi.
Pande zote mbili pia zilijadili ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa, ikiwemo majadiliano yanayohusiana na COP31, ambayo itafanyika nchini Uturuki, alafu mkutano unaofuata ufanyike nchini Ethiopia mwakani.














