Shirikisho la Soka la Ufaransa siku ya Jumanne lilimteua Zinedine Zidane kuwa kocha wa timu ya taifa, akichukua nafasi ya Didier Deschamps ambaye ameinoa timu hiyo kwa miaka 14.
Rais wa Shirikisho Philippe Diallo alisema Zidane aliteuliwa baada ya majadiliano na kamati kuu na akatia saini mkataba wa miaka minne kuanzia Agosti 1.
Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 54 ataanza kusimamia mechi yake ya kwanza Septemba 25 dhidi ya Uturuki kwenye Ligi ya Mataifa ya UEFA.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Zidane alisema amekataa fursa za kuwa kocha kwa miaka mitano iliopita kwa sababu kwake Ufaransa "ndiyo jambo pekee" alilotaka kujihusisha nalo na "ni ndoto kwake."
Zidane anachukua mikoba ya Deschamps, ambaye ameifunza Ufaransa tangu 2012, kuwapa ubingwa wa Kombe la Dunia la FIFA 2018, fainali za Kombe la Dunia 2022, na nusu fainali za Kombe la Dunia 2026 pamoja na fainali za Euro 2016.
Kiungo huyo wa zamani hajakuwa kocha tangu kuondoka Real Madrid 2021.
Alianza ukocha akiwa naibu wa Carlo Ancelotti Real Madrid 2013.
Alipoteuliwa kocha wa Real Madrid 2016, Zidane aliipa klabu hiyo ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo kabla ya kujiuzulu 2018. Alirudi tena 2019 na kuendelea kuwepo huko hadi 2021.
Akiwa mchezaji, Zidane alicheza mechi 108 Ufaransa, na kufunga magoli 31, na pia kushinda taji la Ballon d'Or 1998. Alistaafu kutoka soka la kimataifa baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2006 dhidi ya Italia katika tukio lililomhusisha mchezaji wa safu ya ulinzi wa Italia Marco Materazzi.



















