Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa Uturuki inafanya kila liwezekanalo kulinda mipaka na anga zake, huku mgogoro katika kanda ukiendelea.
“Hatutoacha kitu linapokuja suala la usalama wa mipaka na anga katika nyakati hizi,” alisema Erdogan siku ya Jumatano.
Kiongozi huyo wa Uturuki alisema kuwa nchi yake inafanya kazi kwa ukaribu na NATO na washirika wake, na ilipo tayari kuchukua hatua kwa tishio lolote.
“Uturuki inachukua hatua zote za muhimu kwa kushirikiana na NATO kuchukua hatua pale inapohitajika,” alisema.
Kauli ya Rais Erdogan inakuja mara baada ya NATO kutungua kombora la Iran lililokuwa linaelekea katika anga ya Uturuki, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Uturuki.
Muda mfupi baadaye, Uturuki ikamwita balozi wa Iran nchini humo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan akifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran, Abbas Araghchi.
Onyo kali
Akizungumzia tukio hilo, Erdogan alisema Uturuki ilitoa onyo kali kwa Iran, kuachana na kitendo kama hicho katika siku zijazo.
“Tumeazimia kuhakikisha usalama wan chi yetu kwa kiwango chochote kile,” alisema.
Kulingana na Erdogan, uimarishwaji wa amani wa Uturuki, unahitaji uimarishwaji wa uwezo wa kiusalama.
“Kama taifa tunataka kuishi katika amani na utulivu, ni lazima tuimarishe hilo,” alisema Erdogan.













