| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Tanzania: Dhahabu yenye thamani ya Bilioni 1.2 yakamatwa jijini Dar es Salaam
Waziri wa Madini wa nchi hiyo, Anthony Mavunde amesema dhahabu hiyo ilikamatwa kupitia operesheni maalum ya vyombo vya dola na mamlaka za madini.
Tanzania: Dhahabu yenye thamani ya Bilioni 1.2 yakamatwa jijini Dar es Salaam
Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde.

Serikali ya Tanzania imekamata dhahabu yenye kilo 4.4 na thamani inayokadiriwa kufikia Bilioni 1.2 katika eneo la Kiluvya, Dar es Salaam, ikiwa ilikuwa ikisafirishwa kutoka Kahama, Shinyanga bila kibali halali.

Akizungumza na vyombo vya habari Julai 27, 2026, Waziri wa Madini wa nchi hiyo, Anthony Mavunde amesema dhahabu hiyo ilikamatwa kupitia operesheni maalum ya vyombo vya dola na mamlaka za madini. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, mzigo huo umetaifishwa na sasa ni mali ya serikali, huku ikihifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

"Ndugu zangu, dhahabu hii yenye zaidi ya thamani ya Bilioni 1.2 haikupitia katika mfumo rasmi wa ufanyaji biashara ya madini na hivyo kupelekea Serikali kukosa mapato ambayo yangeisaidia kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi," alieleza Mavunde.

Amesisitiza kuwa, endapo dhahabu hiyo ingetoroshwa na kuuzwa nje ya mfumo rasmi wa biashara ya madini, serikali ya nchi hiyo, ingepoteza zaidi ya Shilingi milioni 108.3 za mapato kutokana na tozo mbalimbali.

“Tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za madini ili kudhibiti utoroshaji na kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na utajiri wa madini nchini,” aliongeza.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili