Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa haki, weledi na heshima, akisisitiza kuwa mapato ya ndai ndiyo msingi wa serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kujenga taifa linalojitegemea.
Akizungumza Julai 01, 2026 wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na utoaji wa Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora, jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema kuwa kodi si adhabu kwa mfanyabiashara wala mzigo kwa mwananchi, bali ni mchango wa moja kwa moja katika huduma za jamii, miundombinu na ustawi wa Watanzania.
“Matamanio yangu ni kuwa na mifumo iliyorahisishwa na inayosomana ya ukusanyaji wa mapato nchini, na watendaji wenye weledi, ubunifu na uadilifu,” alisema Rais Samia.
Hali kadhalika, Rais Samia alisisitiza kuwa vita dhidi ya ukwepaji kodi, magendo na mianya ya upotevu wa mapato, ni lazima viende sambamba na huduma rafiki kwa walipakodi na mazingira bora ya biashara.












