Ghana inatarajiwa kuwa na kongamano muhimu kuhusu ulipaji fidia kwa watumwa mwezi ujao, kufuatia kile maafisa wanachosema kuwa azimio la “kihistoria” la Umoja wa Mataifa kutambua biashara ya utumwa kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.
Kulingana na Shirika la Habari la Ghana, mkutano huo wa siku tatu utafanyika kuanzia Juni 17 hadi 19 jijini Accra na utaongozwa na Rais John Dramani Mahama, ambaye pia anaongoza juhudi za ulipaji fidia katika Umoja wa Afrika.
Hafla hiyo inafuatia kuungwa mkono pakubwa na Umoja wa Mataifa, ambapo mataifa wanachama 123 yalipiga kura kuunga mkono azimio hilo, huku nchi tatu pekee zikipinga —matokeo yanayoonekana kuwa dunia imekubali kuhusu uwajibikaji wa kihistoria.
Katika taarifa kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana, serikali inasema kongamano hilo “litatoa muelekeo wa hatua nyingine ya agenda ya fidia duniani” na kuchagiza majadiliano kimataifa kuhusu haki kwa vizazi vya watumwa wa Kiafrika.
Haki ya fidia
“Kongamano hilo litawaleta pamoja viongozi wa nchi, wanadiplomasia, wanazuoni, wanaharakati na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa,” taarifa hiyo ilisema, kuashiria ushiriki mkubwa katika mkutano huo muhimu.
Maafisa wanasema mkutano huo wa jijini Accra unalenga kuendeleza mjadala zaidi ya kukiri kuelekea katika kuweka mifumo thabiti ya fidia, ikiwemo kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Ghana imejiweka katika nafasi muhimu ya uanaharakati wa kutaka fidia, ikiendeleza msingi uliokuwa awali wa harakati za “Mwaka wa Kurejea Nyumbani” na “Zaidi ya Kurejea”, ambao ulitaka kuunganisha Waafrika wanaoishi nje ya bara kurudi barani.
Kongamano la mwezi Juni linatarajiwa kumalizika kwa kutoa dira au azimio litakaloainisha vipaumbele na mikakati ya haki ya fidia kote duniani.
















