Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka Hamas kuendelea na mpango wa kuwaachilia huru mateka siku moja baada ya kundi la Palestina kutangaza nia yake ya kusitisha mabadilishano ya mateka na wafungwa.
"Lazima tuepuke kwa vyovyote vile kuanza tena kwa mapigano huko Gaza ambayo yangesababisha maafa makubwa," alisema katika taarifa yake Jumanne.
Hamas siku ya Jumatatu ilitangaza kuwa itasitisha mpango wa kuwaachilia mateka wa Israel kwa sasa, ikitowa sababu ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na Israeli, na hivyo kuongeza hatari ya kuanzisha mzozo huo.
Hamas ilitakiwa kuwaachilia mateka zaidi wa Israeli siku ya Jumamosi ili kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina na Wapalestina wengine wanaoshikiliwa katika kizuizi cha Israeli kama ilivyotokea katika muda wa wiki tatu zilizopita.
Ujumbe wa Israeli ulirejea kutoka Doha kwa mazungumzo juu ya awamu inayofuata ya usitishaji vita wa Gaza, ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema Jumatatu, huku kukiwa na mashaka yanayoongezeka juu ya mchakato uliosimamiwa na Misri na Qatar kumaliza vita huko Gaza.
"Pande zote mbili lazima zitii kikamilifu ahadi zao katika makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza tena mazungumzo huko Doha kwa awamu ya pili", Guterres aliongeza.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema Jumatatu kuwa Hamas inapaswa kuwaachilia mateka wote wanaoshikiliwa na kundi hilo huko Gaza ifikapo Jumamosi adhuhuri la sivyo atapendekeza kufuta usitishaji mapigano kati ya Israeli na Hamas na kuzusha machafuko tena.
Afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri ameiambia Reuters siku ya Jumanne kwamba Rais wa Marekani Donald Trump lazima akumbuke kwamba njia pekee ya kuwarudisha nyumbani wafungwa wa Israeli ni kuheshimu usitishaji vita kati ya Israeli na Hamas.