Ufaransa yapinga kukatizwa kwa msaada wa EU kwa Wapalestina

Ufaransa yapinga kukatizwa kwa msaada wa EU kwa Wapalestina

Macron anasema wanachukua hatua kuhakikisha fedha haziwafikii Hamas
Macron anasema wanachukua hatua kuhakikisha fedha hazihamishiwi Hamas / Picha: AFP

Ufaransa imekataa wito wa kusitisha kabisa misaada ya Ulaya kwa watu wa Palestina, huku vita kati ya Hamas na Israel vikiingia siku yake ya nne.

Aidha, Macron anasema kuwa wanachukua hatua kuhakikisha fedha hizo haziwafikii Hamas.

"Hatupendi kusitisha misaada ambayo inawanufaisha moja kwa moja Wapalestina," rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwaambia waandishi wa habari, baada ya mkutano wa pamoja wa baraza la mawaziri la Ufaransa na Ujerumani mjini Hamburg, Ujerumani.

Ameongeza kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa ili kuhakikisha kuwa misaada hiyo ya kibinadamu, iliyokusudiwa kwa Wapalestina, haitumiwi kufadhili shughuli za Hamas.

"Msaada huo unatumika kutoa maji, huduma za afya, chakula na elimu kwa wananchi," alisema.

Macron amesisitiza kuwa hatua dhidi ya ugaidi hazipaswi kulemaza juhudi za kusaidia raia na kushughulikia mahitaji yao ya msingi ya kibinadamu.

"Kwa kweli ninakubaliana na ukaguzi wa misaada yote iliyotolewa na Ulaya, lakini sikubaliani na kusimamisha kabisa kwa fedha,"alisema.

Kwa upande wake, Kansela wa ujerumani Olaf Scholz, alisema kuwa wana hakika kuwa msaada wao wa kifedha hautaenda kwa Hamas, lakini baada ya matukio ya hivi karibuni katika mkoa huo, wataangalia kwa karibu mipango hii ya misaada Kwa Wapalestina.

"Tunazungumza misaada ya kibinadamu, iliyotolewa pia katika maeneo mbali mbali na matukio ya hivi karibuni, ili watu waweze kupata maji na chakula," alisema, akionyesha kuwa miradi ya kibinadamu ilifanywa sio tu huko Gaza, bali pia katika Ukingo wa magharibi West Bank, na pia katika nchi zingine za jirani.

Idadi ya Wapalestina waliouawa na vikosi vya Israeli huko Gaza imeongezeka hadi 765, ikiwa ni pamoja na takriban watoto 143 na wanawake 105, wizara ya afya ya Gaza ilisema mapema Jumanne huku ikiongeza kuwa idadi ya waliojeruhiwa imevuka zaidi ya watu 4,000.

Vile vile, zaidi ya Waisraeli 1,000 wameuawa na wengine zaidi ya 2,600 wamejeruhiwa katika mapigano hayo, Kulingana na wizara ya afya ya Israeli.

AA