Kombe la Urafiki la Uturuki na Serbia, ambalo limekuwa ni utamaduni katika mji mkuu wa Serbia Belgrade tangu 2018, lilifanyika kwa watu walioathiriwa na matetemeko mawili ya ardhi yaliyotokea Uturuki mapema Februari.
Wanachama wa klabu ya waendesha baiskeli ya Uturuki kutoka Mardin, mojawapo ya miji iliyopata madhara kutokana na tetemeko la ardhi, walikuwa wageni maalum katika mbio hizo siku ya Jumapili, ambapo zaidi ya waendesha baiskeli 250 walishiriki.
Balozi wa Uturuki nchini Serbia Hami Aksoy alisema pia walisherehekea Sikukuu ya Kitaifa na Siku ya Watoto na kumbukumbu ya miaka 103 ya kuanzishwa kwa bunge la nchi hiyo.
"Michezo inaleta watu pamoja, inawakusanya sehemu moja. Tutaendelea na shughuli hizi," alisema Aksoy.
Mahusiano ya kirafiki
Katibu wa Jimbo katika Wizara ya Michezo ya Serbia, Marko Keselj, alisema anafurahi kwamba hii ni fursa nyingine na hafla ya kuimarisha uhusiano wa kindugu na wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.
"Kufuatia matetemeko mabaya ya ardhi huko Uturuki, waokoaji wa Serbia na wazima moto wetu walikuwa kati ya watu wa kwanza kuja kusaidia watu wa Uturuki. Kwa hivyo, mbio hizi na hafla zote za michezo zinaweza kuwa moja ya mifano ya jinsi tunavyoimarisha uhusiano wa kirafiki kati yetu,” alisema Keselj.
Raia na mashirika ya kiraia pamoja na serikali ya Serbia waliandaa kampeni nyingi kusaidia wahanga wa tetemeko la Uturuki.
Matetemeko mawili ya ardhi yaliyo tokea tarehe 6 Februari kusini mwa Uturuki yaliua zaidi ya watu 50,000 nchini humo.
Matetemeko hayo yenye ukubwa wa 7.7 na 7.6 yalipiga majimbo 11 ya Uturuki - Adana, Adiyaman, Diyarbakir, Elazig, Hatay, Gaziantep, Kahramanmaras, Kilis, Malatya, Osmaniye na Sanliurfa.
Takriban watu milioni 14 huko Uturuki wameathiriwa na matetemeko hayo.