Takriban wafanyikazi 33 wa Hilali Nyekundu wameuawa huko Gaza tangu Israeli ilipoanzisha vita vyake vya kikatili kwenye eneo lililozingirwa karibu miezi minane iliyopita.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina (PRCS) liliandika kwenye mtandao wa X: " Mazishi ya mwenzetu, Mohammed Jihad Abed, mfanyakazi katika Idara ya Kudhibiti Hatari za Maafa, ambaye aliuawa wakati vikosi vya uvamizi vilishambulia nyumba yake jana usiku huko Rafah."
"Hadi sasa jumla ya wanachama wa PRCS waliouawa tangu kuanza kwa uvamizi huko Gaza imefikia 33, wakiwemo 19 waliouawa walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kibinadamu," iliongeza.
Tarehe 29 Mei, wahudumu wawili wa afya walio na mfungamano na Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, waliuawa katika shambulizi la jeshi la Israeli kwenye gari la wagonjwa lilokuwa njiani kuwahamisha Wapalestina katika kivuko cha Abu al-Said huko Tel al-Sultan katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilisisitiza kuwa Israeli "ililenga wafanyakazi wa afya kimakusudi."
Vita vya ukatili vya Israeli
Israeli imeshambulia Gaza kwa kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7.
Jeshi la Israeli limeshambulia na kuvamia vituo 160 vya huduma za afya huko Gaza na kusababisha kufungwa kwa vituo 55 vya afya na hospitali 33.
Takriban Wapalestina 36,400 wameuawa huko Gaza tangu Israel ianze mashambulizi yake karibu miezi minane iliyopita. Wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto, huku wengine zaidi ya 82,400 wakijeruhiwa, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Maeneo makubwa ya Gaza yamekuwa magofu, huku kizuizi cha Israeli kikisababisha uhaba wa chakula, maji safi na dawa.