Takriban watu 42 wamefariki wakati bwawa lilipovunja kuta zake karibu na mji wa Mai Mahiu, huku mvua kubwa ikinyesha na mafuriko kukumba nchi hiyo.
Bwawa hilo lilipasuka Jumatatu karibu na Mai Mahiu kaunti ya Nakuru, na kusomba nyumba na kupasua barabara, huku waokoaji wakichimba vifusi kutafuta manusura.
"Watu arobaini na wawili wamefariki, ni makadirio ya kwanza. Bado kuna wengine kwenye matope, tunashughulikia kuwaokoa," alisema gavana wa Nakuru Susan Kihika.
Kupasuka kwa bwawa siku ya Jumatatu, kunaongeza idadi ya vifo katika msimu wa mvua wa Machi-Mei hadi 120, na pia kuwa mvua kali isiyo ya kawaida kunyesha Afrika Mashariki, ikichangiwa na muundo wa hali ya hewa wa El Nino.
Wakati huo huo, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema Jumatatu liliopoa miili miwili, baada ya mashua iliyokuwa na "idadi kubwa ya watu" kupinduka wikendi katika kaunti iliyofurika ya Tana River, Mashariki mwa Kenya, na kuongeza idadi ya waliyookolewa kufikia 23.
Kanda za video zilizosambazwa mtandaoni na kutangazwa kwenye runinga zilionyesha mashua iliyojaa watu ikizama, huku watu wakipiga kelele na wengine wakitazama kwa hofu.
Siku ya Jumamosi, maafisa walisema watu 76 wamefariki nchini Kenya tangu mwezi Machi.
Mafuriko makubwa yamesababisha barabara na vitongoji kuzama chini ya maji, na kusababisha zaidi ya watu 130,000 kuyahama makazi yao katika nyumba 24,000, wengi wao katika mji mkuu wa Nairobi, kulingana na takwimu za serikali zilizotolewa Jumamosi.
Shule zimelazimika kufungwa kufuatia likizo za katikati mwa muhula, baada ya wizara ya elimu kutangaza Jumatatu kwamba itaahirisha kufunguliwa kwao kwa wiki moja kutokana na "mvua kubwa inayoendelea".
Machafuko katika kanda
Mvua hizi za masika pia zimesababisha uharibifu mkubwa katika nchi jirani ya Tanzania, ambapo takriban watu 155 wameuawa katika mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Nchini Burundi, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, takriban watu 96,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na miezi kadhaa ya mvua zinazoendelea kunyesha, Umoja wa Mataifa na serikali zilisema mapema mwezi huu.
Uganda pia imekumbwa na dhoruba kali ambazo zimesababisha kingo za mito kupasuka, huku vifo viwili vikithibitishwa na mamia ya wanakijiji kuyahama makazi yao.
Kupasuka kwa bwawa Jumatatu kunakuja miaka sita baada ya ajali sawa na hiyo kutokea katika eneo la Solai kaunti ya Nakuru kuwaua watu 48, na kusababisha mamilioni ya lita za maji yenye matope kupenya kwenye nyumba na kuharibu nyaya za umeme.
Maafa ya Mei 2018 yaliyotokea katika hifadhi ya kibinafsi kwenye shamba la kahawa pia ilitokana na wiki za mvua kubwa iliyosababisha mafuriko mabaya na maporomoko ya matope.
El Nino ni muundo wa hali ya hewa unaotokea kiasili, unaohusishwa na ongezeko la joto duniani kote, na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo ya dunia na mvua kubwa kwingineko.
Mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya watu 300 walikufa kutokana na mvua na mafuriko nchini Kenya, Somalia na Ethiopia, wakati eneo hilo lilipokuwa likikabiliana na ukame mbaya zaidi kutokea katika miongo minne, ukiacha mamilioni ya watu wanaokumbwa na njaa.