na Sylvia Chebet
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ni mtu anayetembea kwenye kamba nyembamba ya kisiasa akiwa anatafuta kupata muhula wa pili na kudumisha ubabe wa chama chake cha African National Congress (ANC).
Kura za maoni zinatabiri kuwa ANC, ambacho kimekuwa madarakani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo mnamo 1994, kinaweza kupoteza wingi wake bungeni, hali ya kusumbua kwa mtu ambaye matumaini yake ya kuchaguliwa tena yanategemea umaarufu wa chama.
Wachambuzi wa siasa wanaamini Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 71, anawakilisha mafanikio na kushindwa kwa chama cha mapambano ya ukombozi, ANC.
David Monyae, profesa msaidizi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, anaiambia TRT Afrika kuwa mafanikio ya ANC yanagubikwa na changamoto zinazokumba wapiga kura wengi nchini Afrika Kusini.
"ANC imefanya mengi kwa viwango vyovyote vile kwa suala la makazi kutokana na muundo wa uchumi wa apartheid na umeme ingawa kampuni ya nishati ya Eskom nchini Afrika Kusini iko na matatizo makubwa kwa suala la mgao wa umeme," Monyae alisema, akibainisha kuwa chama kinakubali bado hakijapiga hatua katika baadhi ya maeneo muhimu.
"Kuhusu ugawaji wa ardhi, msingi wa mapambano ya ukombozi nchini Afrika Kusini, hakuna kitu kikubwa kilichofanyika, kuhusu kushughulikia ukombozi wa kiuchumi wa weusi wengi, hakuna kitu kikubwa kilichofanyika," anabainisha.
"Bado kuna matatizo mengi katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na huduma za afya, elimu na hilo ni sehemu ya lawama kwake (Ramaphosa) kama mkuu wa chama hiki kinachotawala na pia ni sehemu ya urithi wa ANC yote kwa ujumla kwa miaka 30 iliyopita."
Baadhi ya mapungufu yanayopunguza umaarufu wa ANC hata hivyo sio ya Ramaphosa mwenyewe na yanaweza kuhusishwa na watangulizi wake.
Lakini anahukumiwa vikali kwa kushindwa kwa chama kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita tangu alipochukua madaraka.
"Hasa hakuna visingizio linapokuja suala la ufisadi. Hilo limekuwa janga... na yote haya yalitokea chini ya uangalizi wake. Uchumi haujakua, ingawa tulikuwa na janga la ulimwengu na mgogoro wa kifedha wa kimataifa, bado angeweza kufanya vizuri zaidi," Monyae anaamini.
Kiwango cha ukosefu wa ajira, ambacho kimesimama kwa asilimia 32, ni donda jingine kwa ANC ya Ramaphosa lakini rais huyo anayeongoza anaamini kuwa chama kimepata mafanikio ambayo yatakipeleka kushinda tena.
Umeme sasa unapatikana kwa asilimia 93 Afrika Kusini, kutoka asilimia 36 wakati wa utawala wa apartheid ambapo ilikuwa ni haki ya wachache weupe. Lakini mgogoro wa nishati wa muda mrefu unaosababisha mgao wa umeme wa hadi saa 12 kwa siku umeathiri sana shughuli za kiuchumi na kutia doa kwenye picha ya chama.
"Ni mafanikio makubwa lakini bado kuna mengi ya kufanya," Ramaphosa alikiri hivi karibuni.
Rais pia anakubali kuwa wapiga kura wengi "wanaikosoa vikali ANC," lakini ana imani kuwa bado ni chama cha kushinda na yeye, ndiye mgombea anayefaa zaidi.
"Watu wengi ambao wamekuwa wakipigia kura ANC kila wakati bado wanaona ANC kama chombo pekee cha mchakato wa mabadiliko nchini, kuimarisha na kuifanya kuwa bora," alisema Ramaphosa, akiongeza "watu wengi hawaoni mtu mwingine anayefanya vizuri zaidi."
"Hata hivyo, hii inaweza kuwa nafasi ya mwisho kwa ANC," Monyae anasema.
"Bado kuna kizazi cha watu kama mimi ambao wanakumbuka vizuri sana yaliyopita. Bado wana makovu ya utawala wa zamani, na hatujafikia hatua ya kizazi kinachosahau yaliyopita na kwa hivyo, watu wanaiona ANC kama harakati ya ukombozi na kujaribu kuipa nafasi ya pili, nafasi ya tatu."
Pamoja na chama, utu wa Ramaphosa unabaki kuwa kadi yake ya mwitu kulingana na wachambuzi.
Monyae anaamini kuwa licha ya orodha ndefu ya mapungufu, "bado kuna watu wanaosema oh sawa, tunaelewa makosa, tunaelewa yote haya lakini yeye ndiye bora kati ya wabaya."
Akirejea siku za mapambano ya ukombozi na mabadiliko ya baadae kutoka kwa utawala wa ubaguzi wa rangi hadi Afrika Kusini ya kidemokrasia, Ramaphosa, wakili kwa taaluma, anasimama imara kati ya wale wanaotambuliwa kwa kuchangia pakubwa.
"Kwa hakika, yeye ni, kwa kukosa neno bora, mkunga wa demokrasia tunayofurahia. Alikuwa mpatanishi mkuu wa ANC wakati wote wa mazungumzo na utawala wa apartheid na alikuwa kiongozi katika uandishi wa katiba tuliyonayo," Monyae anabainisha.
Mwanaharakati wa zamani wa vyama vya wafanyakazi ambaye aliwakilisha wafanyakazi wa migodi, Ramaphosa alikuwa na ndoto za urais tangu siku ya uhuru lakini ilibidi avumilie kusubiri miaka 25 kabla ya kupanda hadi kilele.
Aliyetangulia kabla yake, Jacob Zuma, alilazimika kujiuzulu baada ya kukabiliwa na msururu wa tuhuma za ufisadi na Ramaphosa - ambaye wakati huo alikuwa makamu wa rais - alipanda kwa wimbi la kupinga Zuma hadi kufikia ikulu.
Lakini katika uchaguzi wa mwezi huu, safari ni ngumu na yenye vikwazo kwa rais anayeongoza. Kura ya hivi karibuni ya kampuni ya tafiti za kura ya maoni, Ipsos, inaonyesha kuwa chama tawala, ambacho kilishinda zaidi ya asilimia 57 ya kura katika uchaguzi wa kitaifa wa 2019, kimepungua hadi zaidi ya asilimia 40.