Uchaguzi wa mwaka huu unaonekana utakuwa na ushindani mkali zaidi tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, huku kura za maoni zikionyesha kuwa chama tawala cha African National Congress ANC kinaweza kupoteza wingi wake kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 madarakani.
Tuwaangalie baadhi ya viongozi walio mstari wa mbele katika kuwakilisha vyama vyao wakati wa kuwania uongozi wa nchi hiyo.
Cyril Ramaphosa
Chama kilichoongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimae kupata uhuru, ANC, kwa sasa kipo madarakani. Ukosefu mkubwa wa ajira, usawa wa kiuchumi unaoendelea, tuhuma za ufisadi, na kukatika kwa umeme mara kwa mara ni matatizo ambayo ANC inayoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa inajaribu kutatua.
Ramaphosa ni mwanasiasa ambaye kwa sasa ni Rais wa nchi hiyo, akiwa madarakani tangu Februari 2018. Alizaliwa tarehe 17 Novemba 1952. Kabla ya kuwa Rais, Ramaphosa alikuwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Jacob Zuma.
Ramaphosa ni kiongozi wa Chama cha African National Congress (ANC) na amekuwa na nafasi muhimu katika siasa za Afrika Kusini kwa muda mrefu. Alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa mapambano dhidi ya ubaguzi na alikuwa katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi cha National Union of Mineworkers (NUM). Pia alihusika katika mazungumzo ya kumaliza ubaguzi wa rangi na aliandika sehemu kubwa ya katiba mpya ya Afrika Kusini baada ya 1994.
Kabla ya kuingia tena kwenye siasa za kitaifa, Ramaphosa alikuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa na alihusishwa na sekta mbalimbali za uchumi, ikiwa ni pamoja na madini, kilimo, na biashara. Uongozi wake umekuwa ukilenga kupambana na ufisadi, kuboresha uchumi, na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ili kupunguza ukosefu wa ajira na kuboresha maisha ya Waafrika Kusini.
Ramaphosa amekabiliana na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na tuhuma za ufisadi ndani ya chama chake na matatizo ya kiuchumi kama vile umeme wa mara kwa mara na ukosefu wa ajira. Hata hivyo, ameendelea kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uwazi, na mageuzi ya kiuchumi ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Kusini.
“Ramaphosa sio mgombea maarufu zaidi wa ANC, lakini anapata nguvu kutokana na ukweli kwamba ANC yenyewe ni kubwa na bado inabaki kuwa maarufu sana,” afafanua Marisa Lourenco, mchambuzi huru wa siasa kutoka Afrika Kusini.
“Bado anaweza kuvutia umati kwa sababu ya jinsi ANC ilivyo, chama daima kinakuja mbele ya rais. Hiyo imekuwa ikitokea na hakika inatokea sasa.”
John Steenhuisen
Chama cha Democratic Alliance (DA), chama kikuu cha upinzani kinachoongozwa na John Steenhuisen, kinaunga mkono uwekezaji zaidi wa kiuchumi na ubinafsishaji. Pamoja na mpango wa kuunda ajira mpya, kumaliza kukatika kwa umeme, pamoja na kupunguza uhalifu kwa asilimia 50.
Steenhuisen alizaliwa tarehe 25 Machi 1976. Steenhuisen alianza kazi yake ya kisiasa katika Baraza la Jiji la Durban na baadaye akachaguliwa kuwa mwanachama wa Bunge la Jimbo la KwaZulu-Natal.
Mwezi Oktoba 2019, baada ya kujiuzulu kwa Mmusi Maimane, Steenhuisen aliteuliwa kuwa kiongozi wa muda wa DA. Aliendelea kuwa kiongozi wa chama hicho baada ya kuchaguliwa rasmi mnamo Novemba 2020. Katika nafasi hii, Steenhuisen ameongoza juhudi za chama chake kupigania sera za kiuchumi huru, kupunguza uhalifu, na kuboresha huduma za msingi kama vile umeme na elimu na kuongeza ajira.
Steenhuisen anajulikana kwa hotuba zake zenye msimamo wa kati na mara nyingi amekuwa akikosoa serikali ya ANC kuhusu masuala ya ufisadi, usimamizi mbovu wa uchumi, na kutokuwepo kwa uwajibikaji.
Gayton Mckenzie
Gayton McKenzie ni mfanyabiashara na mwandishi. Alizaliwa Machi 10, 1974, na anajulikana kwa kuwa mfungwa aliyebadilisha maisha yake baada ya kifungo gerezani.
McKenzie ni kiongozi wa Patriotic Alliance (PA), chama cha siasa alichokianzisha mnamo 2013. PA inazingatia masuala kama vile uwezeshaji wa kiuchumi, haki za kijamii, na kupambana na ufisadi.
McKenzie amekuwa mkosoaji mkubwa wa ufisadi na amekuwa akitetea kuinua jamii zilizo na mazingira magumu. Kazi yake katika siasa imejulikana kwa kauli zake za ujasiri.
“Patriotic Alliance imefanya vizuri sana Gauteng. McKenzie anafanya vizuri katika sehemu za Western Cape pia.”
"Amefanikiwa kupitia mazungumzo na juhudi zake yeye mwenyewe na si chama kwa ujumla. Ameweza kufanya mazungumzo katika maeneo yenye viwango vya juu vya vurugu za magenge, jambo ambalo DA haijafanikiwa kuwa na aina hiyo ya mazungumzo," Lourenco asema.
Julius Malema
Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na Julius Malema, kinapigania mageuzi makubwa ya kiuchumi. Pamoja na kutaifisha benki, migodi, na sekta nyingine muhimu za kiuchumi, EFF inakusudia kugawa ardhi kwa wasiojiweza. Migogoro inayohusisha wanachama wa EFF na vyombo vya usalama imeandikwa.
Malema amezaliwa tarehe 3 Machi 1981. Kabla ya kuanzisha EFF mwaka 2013, Malema alikuwa rais wa Ligi ya Vijana ya African National Congress (ANC) kutoka mwaka 2008 hadi 2012.
Malema anajulikana kwa msimamo wake wa kupigania haki za kiuchumi, hasa kwa wale wasiojiweza, na kwa sera zake za mageuzi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa sekta muhimu kama migodi na benki, na ugawaji wa ardhi. Amekuwa akihusika katika mijadala mingi ya kisiasa nchini Afrika Kusini na ni maarufu kwa matamshi yake makali na uwezo wake wa kujipatia umaarufu kupitia hotuba zenye ushawishi.
Licha ya kuwa na wafuasi wengi, Malema pia amekosolewa na wapinzani wake kwa sera zake ambazo zinachukuliwa kuwa za msimamo mkali na kwa utata unaozunguka maisha yake ya kisiasa na kisheria.
“Julius Malema ana utu na ujasiri mwingi,” ameeleza Lourenco akiongeza “Floyd Trivago pia ni mtu muhimu huko, lakini Malema hakika ndiye maarufu zaidi. Yeye ndiye anaye nukuliwa zaidi na kujulikana. Yeye ndiye anayepewa sikio zaidi na tena, bado anachukuliwa kama mtu anayefaa kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi ya kimapinduzi kama anavyoiita na dhidi ya ukiritimba wa wazungu.”
Herman Mashaba
Herman Mashaba ni mjasiriamali na mwanasiasa aliyezaliwa August 26, 1959. Anajulikana zaidi kama mwanzilishi wa kampuni ya bidhaa za nywele ya Black Like Me, ambayo aliianzisha katika miaka ya 1980 na kuiendeleza kuwa biashara yenye mafanikio.
Alihudumu kama Meya wa Johannesburg kutoka mwaka 2016 hadi 2019, akiwakilisha chama cha Democratic Alliance (DA). Mwaka 2020, alianzisha chama kipya cha siasa kiitwacho ActionSA, ambacho kinazingatia kupambana na ufisadi, ukuaji wa uchumi, na haki za kijamii.
Mashaba anajulikana kwa msimamo wake thabiti juu ya uhuru wa kiuchumi na juhudi zake za kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini nchini Afrika Kusini.
“Chama kinamzunguka sana yeye. Haimaanishi kwamba yeye anahusika na maamuzi yote, lakini anaonekana kama mgombea anayevutia tabaka la kati la weusi na tabaka la kati la wazungu. Anajulikana kwa kauli zake dhidi ya maskini na za chuki dhidi ya wageni,” Mtaalamu Lourenco aeleza.
Mashaba hajazungumziwi sana kwenye vyombo vya habari kuelekea uchaguzi huu, lakini kuna kila ishara ya kwamba ataweza kuvutia kura kwa ajili ya chama chake katika Western Cape.
Jacob Zuma
Rais Ramaphosa alimuondoa rais wa zamani kwenye chama cha ANC, Jacob Zuma, madarakani kwa tuhuma za ufisadi na wafuasi wa Zuma wasioridhika wameunda chama cha uMkhonto weSizwe kinachojulikana kama chama cha MK, mpinzani mpya wa ANC.
Zuma, ambae alizaliwa April 12, 1942 hataweza kushiriki kama mgombea katika uchaguzi huu kwani mahakama kuu nchini Afrika Kusini mnamo Mei 20, 2024, iliamua kwamba Zuma hawezi kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao. Na bado ana umaarufu kwa wananchi wengi nchini.
Lourenco anaeleza kuwa umaarufu wa MK unategemea sana Jacob Zuma, licha ya tuhuma zote za ufisadi na masuala yaliyo thibitishwa. Bado anachukuliwa kama “mtu anayeelewa matatizo ya watu wa hali ya chini, mtu ambaye alitupiliwa mbali na ANC na kama mtu ambaye kwa kweli anaamini katika mabadiliko ya kiuchumi.”
“Ni mtu ambaye ni sahihi sana na anaunga mkono sana vyama vya wafanyakazi. Na yote hayo. Kwa hiyo, ni mtu maarufu sana kwa vyombo vya habari. Lakini hata hivyo, yeye hakika ni mmoja wa watu muhimu zaidi ndani ya chama. Na yeye hakika ni sababu ya umoja,” asema Lourenco.
Mwisho wa siku urais uko hivi…
Lourenco anahitimisha kwa ujasiri kwamba hakuna hata mmoja wa wagombea waliotajwa ambaye ni mgombea anayefaa kwa urais. “Namaanisha, hakuna hata mmoja wao anayefaa kuwa rais, hata makamu wa rais. Mtu pekee ambaye ana fursa ya kuwa rais ni Ramaphosa, iwe ANC itapata zaidi ya asilimia 50 au la.”
Idadi isiyokuwa ya kawaida ya wagombea itakuwa ikigombewa katika uchaguzi ambao utakuwa na karatasi tatu za kupigia kura. Katika duru ya kwanza inayojulikana kama kura ya kitaifa ya fidia, wagombea watagombea tu kama vyama vya siasa kwa viti 200 vya wawakilishi wa kitaifa. Wapiga kura watachagua wawakilishi wa serikali na wa ndani kujaza viti vyengine 200 vya Bunge la Kitaifa katika duru ya pili ya kupiga kura. Wapiga kura katika kila jimbo watachagua wawakilishi wa kutumikia mabunge yao ya majimbo kwenye kura ya majimbo.
Serikali ya kwanza ya muungano inaweza kuundwa kutokana na matokeo ya uchaguzi yatakayobadilisha mazingira ya kisiasa nchini humo. Macho yote yako kwa Afrika Kusini wakati siku ya uchaguzi ikikaribia, ikitarajia mustakabali ambao demokrasia hii yenye nguvu itaamua.
Wagombea wengi waliteuliwa na vyama vya siasa 70, isipokuwa wagombea 11 ambao ni huru. Jumla ya vyama vya siasa 31 vitashiriki katika uchaguzi wa kitaifa kwa mara ya kwanza.
Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) inasema watu milioni 27.79 wamejiandikisha kupiga kura, kutoka milioni 26.74 mwaka 2019.
Takriban vituo vya kupigia kura 23,292 vitakuwa wazi tarehe 29 Mei kuanzia saa 5:00 GMT hadi saa 19:00 GMT.