Apple wanatuhumiwa kutumia madini kutoka maeneo yanayokumbwa na ukiukwaji wa haki za binadamu. / Picha: Reuters

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaishutumu kampuni ya Apple kwa kutumia madini "yanayochimbwa kinyume na sheria" kutoka mashariki mwa nchi hiyo inayokumbwa na mzozo, mawakili wanaoiwakilisha nchi hiyo ya Kiafrika walisema Alhamisi.

Mawakili DRC wameitumia Apple amri ya kuzuia kuendelea au kufanya kazi rasmi ya kusitisha shughuli hiyo, amri ilionya kampuni hiyo kubwa ya teknolojia kwamba huenda ikachukuliwa hatua za kisheria ikiwa madai hayo yataendelea kuripotiwa. Shirika la habari la AFP limeoneshwa amri hilo.

Mawakili hao walishutumu Apple kwa kununua madini yaliyoingizwa kiharamu Rwanda kutoka nchi ya DRC, ambako utoroshaji wa madini unafanyika na kuingizwa katika mnyororo wa ugavi wa kimataifa.

AFP ilipowasiliana na kampuni ya Apple, ilijibu kwa kuonyesha ripoti yake ya kila mwaka ya 2023 inayo angazia matumizi ya madini yenye migogoro ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa bidhaa za teknolojia.

Kuanzishwa upya kwa M23

"Kulingana na uchunguzi wa kina tuliyoifanya, hatukupata uthibitisho wowote wa kuonyesha kuwa 3TG (bati, tantalam, tangsten na dhahabu) zilizochomwa au kusafishwa katika mnyororo wetu... hadi kufika Desemba 31, 2023, kuhusika kwa njia yeyote ile katika kufadhili au kunufaisha vikundi vyenye silaha nchini DRC au nchi jirani," ilisema.

Eneo la Maziwa Makuu lenye utajiri mkubwa wa madini nchini DRC limekumbwa na ghasia tangu vita vya kikanda katika miaka ya 1990, huku hali ya wasiwasi ikipamba moto mwishoni mwa 2021 wakati waasi wa Machi 23 Movement (M23) walipoanza kuteka tena maeneo.

DRC, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zinaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi ya waasi, ikiwa ni pamoja na M23, katika jitihada za kudhibiti rasilimali kubwa za madini katika eneo hilo, madai ambayo Kigali inakanusha.

"Apple imeuza teknolojia iliyotengenezwa kwa madini yanayotokana na eneo ambalo idadi ya watu imeathiriwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu," mawakili wa DRC waliandika.

Bidhaa zilizochafuliwa na damu

Unyanyasaji wa kijinsia na rushwa iliyoenea katika maeneo zinazotoa madini kwa ajili ya matumizi ya kampuni ya Apple ni baadhi tu ya madai yaliyotolewa katika barua hiyo.

Mac, iPhone, na bidhaa zingine za Apple "zinahusika na damu ya watu wa Congo", mawakili wa DRC walisema.

Mawakili wa Ufaransa William Bourdon na Vincent Brengarth walituma amri hiyo rasmi wiki hii kwa kampuni ya teknolojia ya Apple nchini Ufaransa na wakili Robert Amsterdam alituma kwenye makao makuu ya kampuni hio Marekani.

"Apple imekuwa ikitegemea wauzaji wengi ambao hununua madini kutoka Rwanda, nchi maskini ya madini ambayo imekuwa ikiibia DRC na kupora maliasili yake kwa karibu miongo mitatu," waliandika.

Kutengeneza simu mahiri

DRC ina utajiri mkubwa wa tantalamu, bati, tungsten na dhahabu - mara nyingi hujulikana kama 3T au 3TG - madini yote yanayotumika kutengeneza simu mahiri na vifaa vingine vya kielektroniki.

Juhudi za kampuni hiyo kubwa ya kiteknolojia kutafuta madini yake kimaadili "hazitoshi," alisema wakili Bourdon.

"Apple inaonekana kutegemea zaidi umakini wa wasambazaji wake na kujitolea kwao kuheshimu kanuni za maadili za Apple," iliandikwa kwenye amri.

Hata hivyo wasambazaji na wakaguzi wao wa nje wanaonekana kutegemea uthibitisho kutoka kwa Mpango wa Ugavi wa Tin Supply Initiative (ITSCI), "ambao umeonekana kuwa na mapungufu mengi na makubwa," ilisema amri hiyo.

Mpango wa ITSCI ni mojawapo wa mfumo zilizoanzishwa zaidi za miaka kumi iliyopita ili kuhakikisha usambazaji wa madini "yasiyo na migogoro" nchini DRC, kulingana na NGO ya Uingereza ya Global Witness.

Mnamo Aprili 2022, Global Witness ilishutumu ITSCI kwa kuchangia katika utoroshaji wa madini yenye migogoro, kufanyisha watoto kazi, biashara haramu na ulanguzi nchini DRC.

Wabingwa wa teknolojia

Apple sio kampuni kuu pekee inayotegemea mfumo " mbovu ", ilisema Global Witness.

Tesla, Intel, na Samsung ni miongoni mwa makampuni yanayotegemea ITSCI, lakini ripoti ya Global Witness ilifichua kuwa "asilimia tisini ya madini" kutoka maeneo maalum ya uchimbaji madini yaliyopitiwa na mpango huo hayakutoka kwenye migodi iliyoidhinishwa.

Notisi rasmi ya DRC kwa Apple inajumuisha maswali kuhusu "madini 3T yanayotumika katika bidhaa za Apple" na kutaka kampuni hio ya teknolojia ijibu "ndani ya wiki tatu."

"Chaguo zote za kisheria ziko mezani," mawakili hao waliiambia AFP.

Kuongezeka kwa mahitaji ya kobalti na shaba ili kuwezesha nishati safi, kama vile betri zinazoweza kuchajiwa mara kwa mara, pia kumesababisha uhamisho wa lazima, unyanyasaji wa kijinsia, nyumba kuchomwa moto na kupigwa kwa watu mashariki mwa DRC, kulingana na Ripoti ya Kimataifa ya Amnesty ya 2023.

Watu milioni moja wamehama

Wanamgambo wa M23 kwa sasa wanadhibiti maeneo makubwa Kaskazini mwa Kivu na wanaizunguka mji mkuu wa mkoa wa Goma, ambapo zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao kutokana na vita wamejazana katika kambi.

Umoja wa Mataifa ulisema mwaka 2023 kwamba watu wanaoishi mashariki mwa DRC wanakabiliwa na ghasia zisizosikika, na kuzitaja kuwa moja ya "maeneo mabaya zaidi" kwa watoto duniani.

Madini yanasafirishwa hadi Rwanda, kwa ajili ya utoroshaji ili kukwepa vizuizi vilizowekwa kuzuia uuzaji wa "madini yenye kutokana na migogoro," Global Witness imesema.

"Wajibu wa Apple na watengenezaji wengine wakuu wa teknolojia wanapotumia madini yanaopatikana kupitia umwagaji damu kwa muda mrefu haueleweki," mawakili waliambia AFP.

AFP