Watu sita wameuawa nchini Kenya wakati wa maandamano ya Jumatano yaliyoandaliwa na upinzani.
Vifo vitatu kati ya hivyo viliripotiwa Jumatano katika mji wa Mlolongo, takriban kilomita 20 kutoka eneo kuu la biashara la Nairobi.
"Pia tuna vifo vingine viwili huko Kitengela na kimoja huko Emali," afisa wa polisi aliiambia AFP, huku polisi wa pili pia akithibitisha vifo vya watu sita katika miji hiyo mitatu.
Kitengela iko katika Kaunti jirani ya Kajiado, huku Emali iko katika Kaunti ya Makueni.
Upinzani kuhairisha mkutano
Upinzani nchini Kenya ulisitisha mkutano wa kisiasa uliokuwa ufanyike katika uwanja wa Kamukunji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, siku ya Jumatano.
Kiongozi wa muungano wa Azimio, Raila Odinga, alisema wamepokea taarifa za kijasusi kuwa serikali inapanga vitendo vya "madhara" ili kuwafukuza waandamanaji.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kwamba walilazimika kufuta mkutano huo ili kuepusha maafa na uharibifu zaidi.
“Mapema leo asubuhi, wafanyakazi wetu waliokuwa wametumwa kuweka jukwaa huko Kamukunji walishambuliwa na vifaa vyao kuharibiwa. Baadhi walikamatwa,” Odinga alisema katika taarifa yake Jumatano.
"Uamuzi wa kimkakati"
"Ili kuwalinda watu wetu na kuepusha majeraha na kupoteza maisha zaidi, tumefanya uamuzi wa kimkakati wa kutoendelea na mkutano wa hadhara huko Kamkunji leo mchana. Kwa vyovyote vile wananchi wametoa hoja zao,” alisema.
Siku ya Jumanne, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya Japhet Koome alisema watazuia makundi yoyote au maandamano ya upinzani kwa sababu waandamanaji hawakuwa wamewaarifu polisi kabla ya maandamano hayo.
Odinga anaongoza maandamano ya kila wiki nchini Kenya kushinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha na kuachana na Sheria ya Fedha ya 2023, ambayo imeanzisha msururu wa ushuru ambao umesababisha gharama za petroli na usafiri kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Rais William Ruto anashikilia kuwa serikali inahitaji pesa zaidi kwa shughuli za kila siku, ikiwa ni pamoja na matumizi ya kawaida na maendeleo, hivyo basi ushuru unaongezeka.