Mapigano yameongezeka katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, huku vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) vikidai kuwa vimepata udhibiti kamili wa kituo kikuu cha polisi kusini mwa mji mkuu.
Kundi la RSF linasema kuwa limekamata lori 160, magari 75 na vifaru 27 vya polisi.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa limeona picha zilizoonyesha wapiganaji wakihamisha masanduku ya risasi kutoka kwenye ghala na wapiganaji wakisherehekea, lakini hawakuweza kuthibitisha mara moja picha hizo.
Kuongezeka kwa vita
Vikosi vya usalama vya Sudan bado havijatoa maoni yao kuhusu tukio hili la hivi punde.
Miji mitatu ambayo inaunda jiji mkuu mpana - Khartoum, Bahri, na Omdurman - imeshuhudia kuongezeka kwa mapigano tangu Jumamosi wakati mzozo kati ya jeshi na RSF ukiingia wiki yake ya 11.
Wenyeji pia wameripoti kuongezeka kwa kasi kwa ghasia huko Nyala, mji kubwa zaidi katika eneo la magharibi la Darfur.
Ongezeko la hivi punde la mapigano linafuatia mikataba iliyofeli ya kusitisha vita, yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia.
Raia katikati ya mapigano makali
"Kaskazini mwa Omdurman, tumekuwa na mashambulizi ya angani, mizinga ya risasi, pamoja na mashambulizi ya kuzuia ndege za RSF," Mohamed al-Samani mwenye umri wa miaka 47, mkazi, aliiambia Reuters.
Msemaji wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani alitoa wito kwa wapiganaji kutoa usalama kwa watu wanaokimbia El Geneina na kwa wafanyikazi wa misaada.
Hii inafuatia ripoti za wakimbizi kuuawa kati ya jiji hilo na mpaka siku ya Jumamosi.
Takriban watu milioni 2 sasa ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan, na karibu 600,000 wamekimbilia nchi jirani, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.