Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Alhamisi (Disemba 26) alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa wa Msumbiji kutuliza mvutano uliosababisha machafuko ya wenyewe kwa wenyewe yanayohusishwa na uchaguzi wa Oktoba wenye mgogoro.
"Katibu Mkuu ana wasiwasi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi, ambazo zimesababisha kupoteza maisha na uharibifu wa mali ya umma na za watu binafsi," Msemaji wa Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema katika mkutano na waandishi wa habari.
Uamuzi wa siku ya Jumatatu wa Mahakama ya Juu ya Msumbiji wa kuthibitisha ushindi wa chama tawala cha Frelimo katika uchaguzi wa Oktoba umeibua maandamano mapya nchini kote ya makundi ya upinzani na wafuasi wao ambao wanadai kuibiwa kwa kura.
Ghasia za magereza katika mji mkuu wa Msumbiji-Maputo zilisababisha vifo vya watu 33 na 15 kujeruhiwa Disemba 25.
Kamanda Mkuu wa Polisi Bernardino Rafael alilaumu maandamano yaliyofanyika nje ya gereza hilo kwa kuchochea ghasia hizo.
Waziri wa Sheria Helena Kida alikiambia kituo cha televisheni binafsi cha Miramar TV kwamba machafuko hayo yalianzishwa ndani ya gereza hilo na hayana uhusiano wowote na maandamano nje.