Bunge la Uganda limepitisha mswada wa kudhibiti madawa ya kulevya na kisaikolojia wa 2023 ambao miongoni mwa mengine unalenga kuwaokoa wananchi wa Ugnada kutokana na matumizi ya dawa haramu.
"Tuna tatizo la matumizi ya dawa za kulevya nchini. Matumizi mabaya ya dawa za kulevya hayahusu vijana tu, watu wazima wakiwemo pia baadhi ya wazazi wanahusika," Thomas tayebwa naibu wa spika wa bunge ya Uganda amesema.
"Kati ya wagonjwa 7,035 waliolazwa hospitalini mwaka 2022, asili mia 25 waliathiriwa na matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya. Watu wetu wanakabiliwa na matatizo ya kihisia yanayohusishwa na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na unyogovu," Tayenwa ameongezea.
Je, mswada huu unapendekeza nini?
Mtu atapatikana na hatia ya kukutwa na dawa za kulevya , atatozwa faini ya dola 2,675 au mara tatu ya thamani ya soko ya dawa hizo, au kifungo kisichopungua miaka miwili lakini kisichozidi miaka 10.
Kuvuta, kunusa, kutafuna, au aina yoyote ya kutumia dawa za kulevya au dawa za maradhi ya kisaikolojia itasababisha faini isiyopungua dola 128 na isiyozidi dola 640 au kifungo kisichopungua mwaka mmoja lakini kisichozidi miaka mitano.
Wakati huo anayepatikana kuwa mmiliki wa vitu hivyo atapewa faini ya dola 800 au kifungo kisichopungua miaka 3 lakini kisichozidi miaka 5, akipatikana na hatia.
Adhabu hiyo pia itapewa mtu ambaye anamiliki au kusimamia majengo au kuruhusu majengo yatumike kwa matumizi mabaya au utengenezaji, uhifadhi au vyombo vinavyotumika kwa matumizi haramu.
Iwapo utakutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya na vitu vya kisaikolojia, utatozwa faini ya dola 2,675 au mara tatu ya thamani ya soko au kifungo cha maisha.
Adhabu isiyopungua dola 642 au kifungo kisichopungua mwaka 1 na kisichozidi miaka 5 imependekezwa kwa mtu ambaye kwa kujua au ana sababu za kuamini kuwa anashughulikia kifurushi, kontena au kitu chochote ambacho kina dawa za kulevya au vitu vya kuathiri kisaikolojia.
Adhabu kwa wahudumu wa afya
Mswada huu unapendekeza kuwa dakitari wa wanadamu au daktari wa upasuaji wa mifugo anayetumia dawa za kulevya au vitu vya kuathiri kisaikolojia kwa matibabu isiyokuwa inayokusudiwa kwa mgonjwa atatozwa faini ya dola 6,420 au kifungo cha chini ya miaka mitano.
Ili kuepusha matumizi mabaya zaidi ya dawa hizi kwa misingi ya matibabu, serikali ya Uganda imesisitiza haja ya kufutwa usajili wa kitaifa na mashirika ya taaluma ya daktari, daktari wa mifugo, daktari wa meno au mfamasia, ambaye atapatikana na hatia ya kuagiza dawa hizo isivyofaa.