Serikali ya Tanzania imependekeza marekebisho muhimu ya sheria zake za kazi yanayolenga kuimarisha msaada wa afya ya uzazi na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Pendekezo hilo, lilitangazwa kwa mara ya kwanza katika Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi mwezi Mei.
Miongoni mwa mabadiliko hayo, Sehemu ya 33 inapendekeza kuongeza likizo ya uzazi kwa wanawake wanaojifungua kabla ya wakati, kuruhusu akina mama kukaa likizo hadi uja uzito wao ufikie wiki thelathini na sita.
Hatua hii bunge inasema inalenga kusaidia afya na ustawi wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na mama zao.
Sheria ya sasa iko vipi?
Kwa sasa sheria inawaruhusu wafanyakazi wa kike kupata likizo ya uzazi yenye malipo ya siku 84, au siku 100 za likizo yenye malipo ya uzazi ikiwa mfanyakazi atajifungua zaidi ya mtoto mmoja kwa wakati mmoja.
Mfanyakazi anatakiwa kutoa taarifa kwa muajiri kuhusu nia yake ya kuchukua likizo ya uzazi angalau miezi 3 kabla ya tarehe inayotarajiwa ya kuzaliwa na taarifa hiyo inapaswa kuungwa mkono na cheti cha matibabu.
Mfanyakazi wa kike ana haki ya kuanza likizo ya uzazi wakati wowote kuanzia wiki nne kabla ya tarehe inayotarajiwa ya kujifungua, na katika tarehe ya mapema ikiwa daktari atathibitisha kwamba ni muhimu kwa afya ya mfanyakazi au ya mtoto wake ambaye hajazaliwa.
Wafanyakazi wa kike hawaruhusiwi kufanya kazi ndani ya wiki sita baada ya watoto wao kuzaliwa, isipokuwa kama daktari athibitishe kwamba wanastahili kufanya hivyo.
Mfanyakazi ana haki ya kupata likizo ya ziada ya siku 84 juu ya ile likizo ya uzazi yenye malipo ndani ya mzunguko wa likizo ikiwa mtoto atafariki ndani ya mwaka mmoja baada ya kuzaliwa.
Mapendekezo mengine
Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa ni pamoja na Kifungu cha 34A, ambacho kitaruhusu wafanyakazi hadi siku thelathini za likizo bila malipo wakati wa dharura, na Kifungu cha 37, kuzuia waajiri kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa kesi inayomkabili muajiriwa iko kwenye Tume au Mahakama ya Kazi.
Zaidi ya hayo, Vifungu vya 40 na 41A vinapendekeza kiwango cha malipo ya fidia ikiwa muajiriwa atafutwa kazi kwa njia isiyo haki na pia mwongozo wa hatua za kuchukuliwa ikiwa mikataba ya ajira itavunjwa au kukikukwa . Haya yote wabunge wanasema itahakikisha kwamba wafanyakazi wanatendewa haki huku wakitoa ufafanuzi kwa waajiri.
Ikiwa yatapitishwa, marekebisho haya yataashiria hatua endelevu kuelekea kulinda haki za wafanyakazi na kusaidia afya ya uzazi nchini Tanzania.