Spika wa unge la Uganda Rebecca Among amekataa maombi ya Tume ya Fursa Sawa na Utumishi wa Umma ya kutoa ripoti inayoweka wazi malipo (Equal Opportunities Commission & Public Service) ya kutoa ripoti inayoweka wazi mapato ya kila mbunge na watumishi wengine wa chombo hicho.
“Nilipata taarifa kutoka kwa karani wangu ambapo tume hiyo imemwandikia ikitaka ripoti inayoainisha malipo ya kila mbunge, nadhani wamesahau mgawanyo wa madaraka, Bunge la Uganda ni chombo huru, hatuwajibiki kwa tume hiyo," alisema Spika Among.
Kulingana na Among, bunge la nchi hiyo ni chombo huru, huku akimtaka Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, kuikumbusha tume hiyo kuwa malipo ya watumishi wa hayapo kwenye kipengele cha watumishi wa umma.
“Hiyo inajieleza wazi kwenye ibara ya 85, je ni sahihi kwa Tume ya Fursa Sawa kufanya kilicho nje ya majukumu yake na kuanza kuchunguza kisichowahusu," alihoji spika huyo.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo alikubaliana na hoja ya Spika, akisisitiza kuwa tume hiyo ilikuwa inaenda nje ya mipaka ya kazi yake, huku akiahidi kuishauri serikali namna bora ya kukabiliana na suala hilo.
" Majukumu ya Tume hiyo yanaishia kwa makundi waliotengwa kwa misingi ya jinsia, ulemavu wa umri na sababu zingine zilizoundwa na historia, na mila. Nadhani hiyo itakuwa ni kujiongezea tu kazi,” alisema Kiryowa.
Hata hivyo, Ssemujju Nganda mbunge wa Manispaa ya Kira alikataa hoja zilizowasilishwa na Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akisema kuwa Tume ya Fursa Sawa inaweza kuthibitisha udhaifu wa wanachi inapolinganishwa na mishahara inayolipwa na wabunge na wafanyakazi wa Bunge.