Shirika la Ndege ya Uturuki , Turkish Airlines imesimamisha safari za ndege kati ya Johannesburg na Maputo na kati ya Istanbul-Maputo.
Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na hali ya sitoelewana inayoendelea katika eneo hilo kufuatia Mahakama ya Juu zaidi nchini humo kuthibitisha siku ya Jumatatu, ushindi wa chama tawala cha FRELIMO, katika uchaguzi wa urais wa Oktoba. Frelimo imekuwa madarakani tangu mwaka 1975.
Mgombea wa chama tawala cha FRELIMO, Daniel Chapo, alitangazwa mshindi kwa takriban asilimia 65 ya kura, matokeo ambayo yalipingwa na makundi ya upinzani yanayodai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi.
Ongezeko kubwa la uhalifu
Machafuko hayo pia yamesababisha ukiukwaji mkubwa wa usalama, ikiwa ni pamoja na kutoroka kwa watu wengi katika gereza karibu na Maputo ambapo zaidi ya wafungwa 1,500 walikimbia wakati wa ghasia siku ya Jumatano.
Mapigano hayo ndani ya gereza hilo yalisababisha vifo vya watu 33 na wengine 15 kujeruhiwa.
Vifo vya hivi punde vimeongeza idadi ya vifo nchini humo na kufikia 151 tangu Oktoba 21, kulingana na Plataforma Decide, kikundi cha ufuatiliaji wa uchaguzi.
Ongezeko kubwa la uhalifu linatarajiwa katika mji mkuu wa Maputo katika muda wa saa 48 zijazo, alisema Kamanda Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo, Bernardino Rafael.