Mfalme wa kabila la Buganda ni kati ya viongozi 17 wa kimila wanaotambuliwa nchini Uganda  / Picha: AFP

Wizara ya Jinsia inatafuta zaidi ya dola milioni 3.3 (Shilingi bilioni 12.24) kwa ajili ya malipo ya mishahara ya viongozi 17 wa kimila na kitamaduni waliotangazwa kwenye gazeti la serikali, huku kila kiongozi akipangiwa kulipwa dola16,000 ( Shilingi milioni 60) kwa mwezi.

Wizara inahoji kuwa mgawo wa zaidi ya dola 275,927 ( Shilingi bilioni 1.02) katika bajeti ya mwaka ujao utamaanisha kila kiongozi atapata dola 1,300 (Shilingi milioni 5) kwa mwezi, ambayo ni chini ya kile wanachopata sasa.

"Baraza la Mawaziri liliagiza mnamo 2022 kwamba Shilingi milioni 60 zilipwe kila mwezi kwa kila kiongozi wa kitamaduni wote 17 waliotangazwa kwenye gazeti la serikali. Hili lilifanyika mwaka 2024/25, fedha hizi zinalipwa. Hata hivyo katika mwaka ujao wa fedha, Mfumo wa Matumizi ya Muda wa Kati (MTEF) haujatoa kiasi sawa," Agnes Kunihira mbunge anayewakilisha wafanyakazi aliambia Kamati ya bunge ya Bajeti akizungumzia mpango wa bajeti 2025/26.

" Wamerejesha kiasi cha awali cha dola 1,300 (Shilingi milioni 5) ambacho kililipwa kwa kila kiongozi wa kitamaduni kama posho, kiasi cha dola 275,927 (Shilingi bilioni 1.02) pekee kimetolewa. Kwa hiyo tunaomba fedha hizo zirejeshwe kuwa dola milioni 3.3 (Shilingi bilioni 12.24), hii imeacha pengo la dola milioni 3 (Shilingi bilioni 11.4),” alisema Kunihira.

William Wilberforce Kadhumbula Gabula Nadiope IV ndiye mfalme (Kyabazinga ) wa Busoga / picha:  Kyabazinga wa Busoga

Wabunge wengine wamesema hii huenda ikafanya jamii zao kudhani hawawaakilishi vyema bungeni.

"Sijui kwa nini serikali husubiri hadi wakati wa uchaguzi kufanya mabadiliko haya. Je, hiyo inaweza kuwa mbinu ya kutufanya baadhi yetu kuchukiwa na falme za kimila hasa sisi tunaotoka katika falme hizo ambazo ni maarufu," Alex Ruhunda mbunge wa Fort Portal ya kati aliuliza kamati hiyo ya bunge.

" Kwa hiyo nitawaeleza nini watu kwa sababu ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti? Sasa, Baraza la Mawaziri lile lile limewarudisha viongozi wa kimila hadi mapato ya dola 1, 300 kwa mwezi ?” Ruhunda aliongezea.

Mnamo Aprili 2024, Bunge liliidhinisha ombi la Wizara ya Jinsia la kutoa zaidi ya dola milioni 8,47 (Shilingi bilioni 31.330) kwa malipo ya kila mwezi ya dola16,000 (Shilingi milioni 60) kwa kiongozi wa kimila aliyetangazwa kwenye gazeti la serikali na fedha zaidi dola milioni 4.6 (Shilingi bilioni 17.2) kwa ajili ya ujenzi wa majumba ya falme za lteso, Tieng Adhola, Buruli na Rwenzururu.

Hili lilikuwa agizo la Rais Yoweri Museveni.

TRT Afrika