Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa ana maelezo ya kutosha kuthibitisha kuwa wale waliopanga kufanya maandamano nchini siku ya Jumanne Julai 23, walifadhiliwa na vyanzo vya nje.
Takriban watu 45 walizuiliwa na maafisa wa usalama baada ya kukamatwa 23 Julai 2024, baada ya kujaribu kuandamana kwenda bungeni kama ishara ya kupinga ufisadi nchini.
Idadi hii imetolewa na shirika lisilo la serikali linaloitwa Chapter Four. Shirika hili linatetea haki za binadamu na kutoa huduma za kisheria kwa wafungwa.
Lakini Rais Museveni amekashifu waandamanaji.
"Maandamano hayo, yalikuwa na mambo mawili mabaya. cha kwanza, kilikuwa ni ufadhili kutoka kwa vyanzo vya nje ambavyo kila mara vinaingilia masuala ya ndani ya Afrika kwa miaka 600 iliyopita," Rais Museveni amesema katika taarifa yake.
"Wote wanaohusika wanapaswa kujua kwamba Uganda sio ukoloni mamboleo ambapo mipango hiyo isiyo na kina inaweza kutumwa," Rais amesema.
Rais Museveni anadai kuwa waandamanaji walikuwa na nia mbaya.
"Jambo la pili, ni kwamba baadhi ya waandishi na washiriki wa maandamano hayo, walikuwa wakipanga, mambo mabaya sana dhidi ya watu wa Uganda. Mambo mabaya sana hayo, yatajitokeza mahakamani wakati waliokamatwa watakapofunguliwa kesi," Rais Museveni ameongeza.
Rais huyo amesema kuwa inawezekana, kwamba baadhi ya washiriki, hawakujua kuhusu fedha zilizopangwa kutoka nje na mambo mabaya yaliyopangwa. Akidai kuwa ndio maana, walipaswa kusikiliza ushauri wa polisi, sio kuendelea na maandamano.
Lakini walipuuza ushauri wa polisi.
"Ushahidi ulio mahakamani utawashtua wengi. Kama nilivyosema hapo juu, wapangaji wa maandamano haya walitaka kufanya mambo mabaya sana. Shtaka la Polisi la "uvivu na fujo," ninashuku, lilitumika kwa sababu maafisa wa polisi waliotumwa hawakuwa na habari zote. Hii ilikuwa operesheni ya hali ya juu, inayoongozwa na akili. Nina habari nyingi," Rais huyo ametishia.
Rais ametoa uhakikisho kuwa anaongoza vita dhidi ya ufisadi, na anachongoja tu ni ushahidi wa kutosha dhidi ya watu kadhaa.