Bei ya kukodisha ndege binafsi ya kifahari ambayo Rais Ruto alitumia na ujumbe wake inakadiriwa kuwa dola milioni $1.5, kwa mujibu wa ripoti/ Picha: Rachel Ruto

Rais William Ruto wa Kenya amejitetea kuhusu matumizi ya usafiri aliotumia kwenda nchini Marekani katika ziara yake rasmi kutoka 20 hadi 24 Mei 2024.

Mjadala umekuwepo huku wengi wakimlaumu vikali baada ya kusema kuwa ndege ya kibinafsi aliyokuwa amesafiria hadi Marekani wiki jana ilikuwa ya bei nafuu kuliko angetumia Shirika la Ndege la Taifa.

Hata hivyo, Rais Ruto amejitetea.

"Nilipoona mjadala wa jinsi nilivyosafiri kwenda Marekani, na kulikuwa na takwimu za kila aina kuwa 'hii ndege ni kubwa hivi wengine wakisema google hapa na google pale," Rais Ruto alisema katika hotuba yake wakati wa maombi ya taifa ya bunge ambayo hufanyika kila mwaka.

Bei ya kukodisha ndege binafsi ya kifahari ambayo Rais Ruto alitumia na ujumbe wake inakadiriwa kuwa dola milioni $1.5, kwa mujibu wa ripoti.

"(Wengine walidai) hii lazima itagharimu milioni 200 kwa sababu Rais alihitaji kufika kwa starehe akiwa amemshika Rachel mkono. Mimi ni kiongozi aliyewajibika sana, sasa kuna njia naweza kutumia milioni 200," Ruto aliongezea.

"Naomba nifichue hapa kwamba iligharimu Jamhuri ya Kenya chini ya milioni 10 ($76,000) kwa sababu mimi si mwendawazimu. Nilipoambiwa ndege ya bei nafuu ilikuwa milioni 70 ($537,428) niliiambia ofisi yangu wakanunue tiketi za Kenya Airways," ameendelea kufafanua.

Rais Ruto amedai kuwa alipata ndege kwa bei nafuu kutoka kwa marafiki zake, ambao hajawataja.

"Marafiki zangu waliposikia kuwa naenda kusafiri na Kenya Airways na ...baadhi yao waliniambia unataka kulipa kiasi gani nikasema siko tayari kulipa zaidi ya milioni 20 ($153.550) wakasema leta milioni 10 ($76,000), " Rais Ruto ameongeza kusema.

TRT Afrika