Rais William Ruto, ambae ameongoza tukio hilo la kihistoria, ameonyesha matumaini yake ya kufanya kazi na Naibu Rais wake mpya/ Picha: Wengine 

Naibu Rais mpya wa Kenya Kithure Kindiki ameahidi kutoa ushirikiano kwa Rais William Ruto wa Kenya ili kuipeleka nchi katika ngazi ya nyengine.

Kithure ameyasema hayo, mapema hii leo, baada ya sherehe za kuapishwa kama Naibu Rais mpya.

“Rais, nitahudumu chini yako na kukupa usaidizi unaohitaji ili kuipeleka nchi katika ngazi nyingine . Nitakuwa mwaminifu,” amesema Kindiki, mbele ya wageni mbalimbali waliojitokeza katika sherehe hiyo.

Kithure Kindiki, msomi ambae amekuwa katika ulingo wa siasa kwa takriban muongo mmoja/ Picha: Reuters 

Miongoni mwa wageni hao, ni mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Kindiki amapishwa baada ya bunge la Seneti kuunga mkono kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Kwa upande wake, Rais William Ruto, ambae ameongoza tukio hilo la kihistoria, ameonyesha matumaini yake ya kufanya kazi na Naibu Rais wake mpya.

"Ninajivunia kushuhudia kuapishwa kwa Naibu Rais Kithure Kindiki. Yeye ni msomi aliyehitimu sana na bora, wakili na mtumishi wa umma ambaye taaluma yake imefafanuliwa na mafanikio ya mfano ambayo yanaonyesha maono yake ya mabadiliko chanya na kujitolea kwa viwango vya juu vya ufanisi katika majukumu yake,” amesema Rais Ruto.

Kithure Kindiki, msomi ambae amekuwa katika ulingo wa siasa kwa takriban muongo mmoja, anaingia katika historia ya kuwa Naibu Rais wa tatu tangu nchi hiyo kupata katiba mpya mwaka 2010 ambayo ilibadilisha mchakato wa kumpata na kumuondoa Naibu Rais.

Kindiki kabla ya uteuzi wake, alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Itakumbukwa kwamba, uteuzi wake, umefuatia mchakato mrefu wa kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambae wa mswada wa kumuondoa uliowasilishwa katika Bunge la Taifa na lile la Seneti, alituhumiwa kwa mashtaka kadhaa ikiwemo kudharau mamlaka ya Rais.

Hata hivyo, Rigathi pamoja na jopo lake la wanasheria wamepiga tuhuma hizo.

Mpaka sasa, bado haijafahamika ni hatua gani Rigathi atachukua, licha ya kuwepo kwa kesi mahakamani ambayo itaamua iwapo kuondolewa kwake kumefuata sheria au la.

Mapema hii leo, mke wa Gachagua, Dorcas Gachagua aliweka picha katika mtandao wa X ilimuonyesha kiongozi huyo akiwa na familia yake katika bustani.

Dorcas aliandika, “Leo, mimi na familia yangu tunachagua kutoa sala ya kushukuru, tukielewa kwamba, Mungu anabaki kuwa mwenye enzi, iwe anatuokoa ... na moto au la."

TRT Afrika