Mkutano umesimamiwa na Umoja wa Afrika./ Picha AU 

Serikali ya Ethiopia na viongozi wa eneo lake la kaskazini, Tigray, wa chama cha Tigray People Liberation Front, zimefanya mkutano wa kuangalia utekelezaji wa makubaliano ya amani waliotia saini kumaliza vita kaskazini mwa nchi.

Makubaliano hayo yalifanyika mwaka 2022 mjini Pretoria nchini Afrika Kusini, kati ya wanajeshi wa jeshi la taifa na kikundi cha wapiganaji wa Tigray. Vita hivyo vilianza Novemba 2020 wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipotangaza kuwa wanajeshi waliokuwa Tigray walishambulia eneo la kuhifadhi silaha ya taifa.

Upande wa serikali ya Ethiopia katika mkutano na viongozi wa muda wa Tigray.  Picha/AU 

Mkutano wa kuangalia makubaliano hayo sasa unafanyika chini ya uongozi wa Umoja wa Afrika, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyekuwa mpatanishi wa makubaliano hayo amehudhuria mkutano huu.

Baraza la Amani na Usalama la AU linasema mkutano huo unalenga "kutafakari kimkakati na kuunga mkono vipengele muhimu vya Mchakato wa Amani wa Ethiopia, kama vile usaidizi wa kibinadamu, uondoaji wa silaha, ukarabati na ujenzi upya."

Viongozi wa muda wa Tigray katika mkutano wao na serikali ya Ethiopia/ picha AU 

katika miaka miwili ya vita takriban watu 600,000 wanakadiriwa kupoteza maisha yao na mamilioni kulazimika kuhama. Wengine walikimbilia nchi jirani kama Sudan.

Mkutano huu unakuja katika hatua muhimu wakati tofauti kati ya serikali ya shirikisho na utawala wa muda wa Tigray zinaongezeka kwa ajili ya majukumu ambayo hayajatimizwa yaliyotajwa katika makubaliano ya kusitisha vita.

Kuna changamoto kubwa haswa juu ya hali ambayo haijatatuliwa ya Magharibi mwa nchi na sehemu za Tigray Kusini, ambazo bado zinakaliwa na vikosi vinavyoshirikiana na serikali kutoka eneo jirani la Amhara, na matokeo yake ni kuchelewa kurejea kwa waliolazimika kuhama makaazi yao .

Pia bado kuna mvutano kuhusu kuondoka kwa vikosi vya Eritrea.

Serikali imesema gharama ya ujenzi mpya katika eneo la kaskazini lililokumbwa na vita inakadiriwa kuwa dola bilioni 20.

TRT Afrika