Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) Meja Jenerali Aphaxard Kiugu alikutana Jumatatu, na makamanda wa kikosi cha Wanajeshi wa EACRF waliotumwa kudumisha amani Kivu Kaskazini, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilituma wanajeshi kwa mara ya kwanza katika eneo hilo lenye hali tete nchini DRC mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23.
Makamanda waliokutana wametoka vikosi vya Burundi, Kenya, Sudan Kusini na Uganda walijadiliana na kamanda wa kikosi kuhusu hali ya usalama ilivyo sasa katika maeneo yao ya operesheni.
Meja Jenerali Kiugu alizingatia kuongezeka kwa propaganda dhidi ya kikosi hicho na kuwataka makamanda wasibabaishwe bali wawe imara katika kutekeleza majukumu ya EACRF.
Alisisitiza haja ya kuwa na umakini wa ziada na kuhakikisha wanajeshi wanalindwa dhidi ya vitisho vinavyowezekana kutokea kwasababu ya propaganda hizi.
Maeneo haya ya kaskazini mwa DRC ni maeneo ambapo mashambulizi kutoka kwa vikundi vyenye silaha, yanaendelea kutishia juhudi za amani na utulivu zilizopatikana hadi sasa.
Hata hivyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema vikosi vya Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) vitaondoka nchini kufikia tarehe 8 Disemba.
Imekataa kikosi hicho kuongeza muda zaidi ikidai wanajeshi wa Afrika Mashariki hawajaweza kutatua tatizo ya ukosefu wa usalama hasa lile la mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23.