Serikali ya Kaunti ya Machakos nchini Kenya imekataa kuwalipa madaktari waliogoma/ Picha: Wengine 

Serikali ya Kaunti ya Machakos nchini Kenya imekataa kuwalipa madaktari waliogoma ikisema hawatapata pesa yoyote hadi warudi kazini.

Akizungumza katika ziara yake ya maendeleo katika Kaunti ndogo ya Mwala, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti alisisitiza kuwa mahakama imetangaza mgomo huo kuwa haramu na kwamba serikali haitawalipa madaktari fidia kwa kukiuka sheria.

Gavana Ndeti alibainisha kuwa kaunti hiyo imetimiza mahitaji mengi ya madaktari, isipokuwa nyongeza ya mishahara, ambayo alisema kuwa haiwezi kutekelezwa kwa hali ya sasa.

Afisa Mkuu wa Huduma za Kiafya Justus Kasiva alisema wauguzi na maafisa wa kliniki wamerejea kazini lakini madaktari bado wamekaidi.

Alisema hawajawalipa madaktari waliogoma mwezi huu na hatawalipwa iwapo wataendelea kugoma.

Naibu Gavana wa kaunti hiyo Francis Mwangangi alisema kuwa wahudumu 422 wa afya katika kaunti hiyo wamepandishwa vyeo tangu Gavana Ndeti achukue wadhifa huo na kwa hivyo, itakuwa si haki kwa serikali ya kaunti kuendelea kuwapandisha vyeo sehemu fulani pekee.

Naibu gavana huyo alisema mapato yanayogawiwa kutoka kwa serikali ya kitaifa hadi kaunti hayatoshi kukidhi nyongeza ya mishahara na kuwataka wabunge kushinikiza nyongeza ya Sh380 bilioni za sasa.

TRT Afrika