Zahma ilizuka Jumamosi usiku katika uwanja wa Nairobi Polo Club Nairobi, ambako kulifanyika tamasha ya Furaha City.
Mashabiki wa muziki waliachwa vinywa wazi baada ya kizaazaa kutokea kati ya timu ya msanii wa Tanzania Diamond Platinumz na wasimamizi wa msanii wa Kenya Willy Paul kukaribia kushikana mashati dakika chache kabla ya kupanda jukwaani.
Baada ya vuta nikuvute msanii huyo wa Komasava, alirudi kwenye gari lake na kuondoka tamashani bila kutumbuiza akiwa amejawa na ghadhabu na kudai kukosewa heshima.
'Jukwaa ni langu sio lako'
Kilichotokea ambacho kiliwashangaza wengi, wasanii hao walionekana kuzozania ngazi ya kupanda jukwaani.
Kwa mujibu wa walioshuhudia mvutano huo, MC alikuwa akifuata ratiba ya wasanii wanavyoingia jukwaani, na alipomuita Willy Paul ambaye alipangiwa kutumbuiza kabla ya kumpisha Diamond, bingwa huyo wa Bongo Flava kutoka nchi jirani Tanzania aling'ang'ania kutumia wakati huo uliko kusubiri baada ya Willy Paul.
Naye Msanii huyo aliyeangusha vibao kama 'Keroro' na 'Kitanzi' miongoni mwa zingine alikatalia jukwaa huku akionekana kuungwa mkono na mashabiki waliopiga kelele wakiita 'Poze!', kumaanisha wanamtaka Willy Paul.
Diamond alikuwa msanii rasmi wa usiku huo kwahiyo alitarajiwa kutumbuiza wa mwisho.
Tamko la waandaaji
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa mtandaoni ambao wasanii wa muziki na mashabiki kutoka Kenya wengi wamemlaumu Diamond kwa kutoheshimu ratiba, na hasa kwa kukataa kutumbuiza na kuondoka tamashani.
Wengi wamezungumzia tukio hili wakiwemo baadhi ya wasanii wa Kenya walioonyesha kuridhishwa na mashabiki wa Kenya waliosimama kidete kumtetea Willy paul.
Lakini waandaaji wa tamasha wameelezea kutoridhishwa na tukio hilo. Katika taarifa ikyosambazwa mitandaoni, timu ya Furaha City waliwaomba radhi mashabiki na wasanii wengine waliofanikisha tamasha.
Pia walielezea kuwa kwa upande wao walijitahidi bila mafanikio kutuliza hasira za wahusika.
Kama waandaaji tumefanya kila kitu chini ya uwezo wetu kumtimizia Diamond na kikosi chake matakwa yao yote kwa kuzingatia itifaki na maslahi. Lakini tabia ya wasimamizi wake na matakwa yao yalikuwa ya kusikitisha na yasiyo ya kawaida....
Mashabiki walikuwa wamelipa KSh 4,000 kwa tikiti za kawaida, KSh 15,000 kwa VIP na KSh 25,000 kwa VVIP
Wasanii wengine kutoka Tanzania walifanikiwa kutumbuiza akiwemo Zuchu, Rayvanny miongoni mwa wasanii wengine mashuhuri wa Kenya wakiwemo Calligraph Jones, Mejja, Femi one, Claudia Naisabwa na wengineo.
Kufikia Jumapili mchana timu ya Diamond haijatoa tamko lolote juu ya tukio hilo.