Waendesha mashtaka wa Kenya wamesema wanakusudia kumfungulia mashtaka Paul Mackenzie mshukiwa wa kikundi cha dini, na washukiwa wengine kwa mauaji na ugaidi kutokana na vifo vya zaidi ya wafuasi wake 400.
Aliyejiita kasisi Paul Nthenge Mackenzie anadaiwa kuwachochea wafuasi wake kufa kwa njaa ili "kukutana na Yesu" kisa kilichoshangaza ulimwengu.
Mackenzie alikamatwa Aprili mwaka jana baada ya miili kugunduliwa katika msitu karibu na pwani ya Bahari ya Hindi.
Muda wa kuzuiliwa kwake kabla ya kesi umeongezwa mara kadhaa huku uchunguzi ukiendelea.
“Baada ya uchambuzi wa kina wa ushahidi huo, mkurugenzi wa mashtaka ameridhika kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki washukiwa 95,” ofisi ya mwendesha mashtaka ( ODPP) ilisema.
Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya mahakama kuipa mamlaka siku 14 kumfungulia mashtaka dereva huyo wa zamani wa teksi au kumwachilia huru.
Mackenzie na washtakiwa wenzake watakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo mauaji, kuua bila kukusudia na ugaidi.
Pia watashtakiwa kwa "kumtesa mtoto," waendesha mashtaka walisema.
Haijabainika mara moja ni lini washukiwa hao 95 wangefika mahakamani lakini waendesha mashtaka walisema walijitolea "kuwasilisha kwa haraka masuala hayo."
Kunyongwa au kulazimishwa kukosa hewa
Uchunguzi wa maiti umefichua kuwa wengi wa waathiriwa walikufa kwa njaa. Lakini wengine, wakiwemo watoto, wanaonekana kunyongwa, kupigwa au kukosa hewa.
Hadi sasa miili 429 imepatikana. Ugunduzi huo mbaya, katika kile kinachojulikana kama "mauaji ya msitu wa Shakahola," ulisababisha serikali kuashiria hitaji la udhibiti mkali wa madhehebu tofauti.
Kenya ina historia ya kujitangaza kuwa na idadi kubwa ya wachungaji. Taifa lenye Wakristo wengi, Kenya imetatizika kudhibiti makanisa na madhehebu yasiyofaa ambayo yanajihusisha na uhalifu.
Kuna zaidi ya makanisa 4,000 yaliyosajiliwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye watu milioni 53, kulingana na takwimu za serikali.