Akaunti ya X ya Huduma ya Taifa ya Polisi Kenya imeonesha kuwa 11 Septemba 2024 Masengeli alikamilisha ziara yake ya siku tatu ya usalama katika Kaunti za Kaskazini Mashariki mwa nchi/ Picha: National Police Service Kenya 

Kaimu Inspekta Jenerali wa polsi nchini Kenya, Gilbert Masengeli amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela.

Hii ni baada ya kiongozi huyo wa polisi kudharau wito wa mahakama kwa mara saba mfululizo.

" Bwana Masengeli anaamriwa kujisalimisha kwa Kamishna Jenerali wa Magereza ili kuhakikisha kuwa anawekwa gerezani tayari kutumikia kifungo chake," alisema Jaji Lawrence Mugambi.

Masengeli alitarajiwa kufika mahakamani kulingana na amri ya Jaji Lawrence Mugambi.

Masengeli alitakiwa kuieleza Mahakama kuhusu madai ya kutekwa kutekwa nyara kwa ndugu wawili na mwanaharakati mmoja, kwa kipindi cha wiki mbili.

Kaimu Inspekta huyo ameagizwa kufika mbele ya hakimu ana kwa ana kueleza ni kwa nini wanaume hao watatu waliotekwa nyara huko Kitengela, Nairobi hawajaachiwa hadi sasa.

Inadaiwa kuwa, ndugu wawili Jamil Longton, Aslam Longton na mwanaharakati Brian Njagi walichukuliwa kinguvu na watu waliovalia suti, wanaodaiwa kuwa maofisa wa Polisi kutoka Nairobi, huku wakishindwa kutoa sababu za kuwakamata.

" Iwapo atashindwa kujisalimisha gerezani, Waziri wa Mambo ya Ndani lazima achukue hatua zote za kisheria kuhakikisha kuwa bwana Masengeli anafungwa jela ili kutumikia kifungo chake," aliongeza Jaji huyo.

Kulingana na Jaji Mugambi, amri hiyo ni ya shuruti na si adhabu.

" Katika hali ambayo Masengeli anaweza kuepuka kutumikia kifungo hiki na kwa maana mahakama inaweza kusitisha kifungo hiki kwa siku 7 pekee. Kaimu Insepkta wa Polisi anaweza kujisalimisha mbele ya mahakama, hii ana kwa ana kujibu masuala ambayo amekuwa akiyakwepa," alisema Jaji Mugambi.

Ripoti na picha kutoka akaunti ya X ya Huduma ya Taifa ya Polisi Kenya za Septemba 11, 2024 zinamuonesha Masengeli akikamilisha ziara yake ya siku tatu ya usalama katika Kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

TRT Afrika