Kituo hicho cha Nairobi Funeral home ( zamani kiliitwa Nairobi City Mortuary)  ambacho kwa sasa kina zaidi ya miili 600, iilhali uwezo wake ni kuhifadhi miili 184/ Picha:  Wengine 

Kaunti ya Nairobi, nchini Kenya imetoa wito kwa wananchi kuja kuchukua miili ya familia zao katika chumba cha kuhifadhia maiti cha jiji yaani Nairobi Funeral Home. Imeonya kuwa chumba hicho kwa sasa kimejaa.

"Chumba hicho kimepita uwezo wake, na sasa ni sharti kwa umma kuwatambua jamaa zao walioaga dunia ili kutoa nafasi. Kaunti ya Jiji la Nairobi pia inaomba idhini ya mahakama ili kutupilia mbali maiti hizo ambazo hazijadaiwa," ilisoma taarifa kutoka kaunti.

Rufaa ya kaunti inakuja huku kukiwa na mzozo mkubwa wa uwezo katika kituo hicho, ambacho kwa sasa kina zaidi ya miili 600, inayozidi uwezo wake wa 184.

Kaunti hiyo ilisema kuwa majaribio yake ya kupata kibali cha kisheria cha kuiwezesha kutupa miili ambayo haijadaiwa yamecheleweshwa.

Sheria ya Afya ya Umma ya kaunti ya Nairobi, sura ya 242, inasema kuwa miili lazima itunzwe kwa angalau miezi mitatu kabla ya mahakama kuamuru itupwe.

Sheria pia inaamuru notisi kwa umma ya siku 14 kabla ya hatua yoyote zaidi kuchukuliwa.

Taarifa ya kaunti imesema tayari imeiarifu ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na kesi hiyo itasikizwa na Mahakama ya Milimani mnamo Oktoba 15, 2024. Nia kuu ni kaunti kuomba ruhusa ya mahakama ya kuondoa miili ambayo haijadaiwa.

TRT Afrika