Wanamgambo wa Al-Shabaab wamekamata helikopta ya Umoja wa Mataifa katikati mwa Somalia baada ya kutua kimakosa katika eneo linalodhibitiwa na kundi hilo la kigaidi, afisa mmoja alisema.
Helikopta hiyo iliondoka kutoka jiji la Beledwayne na ilikuwa ikielekea katika mji uliokombolewa hivi karibuni wa Wisil katika jimbo la Galmudug nchini Somalia siku ya Jumatano.
Mohamed Abdi Adan, Waziri wa Usalama wa jimbo la Galmudug, alithibitisha tukio hilo, akisema helikopta hiyo ilitua katika eneo la Hindhere katika eneo la Galgadud kutokana na hitilafu ya kiufundi.
Helikopta hiyo ilikuwa imebeba abiria tisa, wakiwemo wafanyakazi wa misaada, wanajeshi, pamoja na maafisa wengine.
Sita kati yao, wamechukuliwa mateka na wanamgambo wa Al-Shabaab, huku wengine wawili wakifanikiwa kutoroka, hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa usalama walioiambia Anadolu kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na vikwazo vya kuzungumza na vyombo vya habari.
Helikopta hiyo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.