Somalia inakabiliwa na baa la njaa ambalo huenda likasababisha ukame iwapo fedha zaidi hazitopatikana kwa haraka, shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya siku ya Ijumaa.
Misimu miwili ya mvua ambayo haikuwa mizuri, mapigano, na mamilioni ya watu kuondoka katika makazi yao yamesababisha kuwepo kwa ukosefu wa chakula, Mkurugenzi wa masuala ya Dharura wa WFP Ross Smith amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.
Karibu watu milioni 4.4, karibu robo ya idadi ya watu nchini humo, watakabiliwa na viwango tofauti vya njaa au zaidi, alionya.
Kulingana na mkurugenzi wa masuala ya dharura, msaada wa vyakula muhimu na lishe wa WFP huenda ukamalizika “katika wiki chache zijazo” iwapo msaada zaidi hautopatikana.
Karibu watoto milioni 2 wana utapiamlo, ikiwemo 400,000 wenye kiwango cha juu zaidi cha utapiamlo. Watu nusu milioni wameondoka katika makazi yao kwenye kipindi cha miezi mitano iliopita, kulingana na WFP.
Kupungua kwa misaada ya fedha kumesababisha kupunguzwa kwa migao kwa sehemu kubwa. Kwa sasa WFP inasaidia watu karibu 640,000, kutoka watu milioni 2.2 kwa mwaka, Smith alisema, na msaada wa lishe kwa wajawazito na watoto umepungua kwa zaidi ya asilimia 75.
“Tuko katika kipindi cha kufanya maamuzi muhimu wakati huu,” amesema Smith. “Bila kuchukuwa hatua, inaweza kuwa tatizo kuwafikia wale walio na shida zaidi kwa wakati ufaao, wengi wao wanawake na watoto.”
Shirika hilo limeonya kuwa kwa mara nyingine tena Somalia inakabiliwa na tatizo la ukame kama miaka iliopita, likieleza kuhusu dalili kama zilizojitokeza kabla ya ukame wa mwaka 2011 na viwango vya karibu kufikia ukame 2022, ambao ulifanikiwa kuepukwa kutokana na misaada kutolewa kwa watu.
WFP inasema ina uwezo wa kukabiliana na hali ila inahitaji msaada wa kifedha haraka ili kuepuka janga.





















