| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Watu wasiopungua 25 wauawa katika shambulio linaloshukiwa kutekelezwa na Boko Haram nchini Nigeria
Gavana wa jimbo la Adamawa, Adamu Umaru Fintiri amelaani shambulizi hilo huku maafisa wa eneo hilo wakisema shughuli za kutafuta miili zinaendelea.
Watu wasiopungua 25 wauawa katika shambulio linaloshukiwa kutekelezwa na Boko Haram nchini Nigeria
Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana na magaidi wa Boko Haram tangu 2009. / / Reuters
tokea masaa 3

Watu wasiopungua 25 waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi katika jimbo la Adamawa, kaskazini-mashariki mwa Nigeria, shirika la habari la AFP limeripoti likinukuu maafisa wa eneo hilo.

Mashambulizi hayo katika miji ya Madagali na Hong, iliyoko karibu na mpaka wa Cameroon, yalihusishwa na magaidi wa Boko Haram, ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika eneo hilo tangu kundi hilo lilipoanza shughuli zake mwaka 2009.

“Watu wenye bunduki tunaodhani ni Boko Haram waliokuwa kwenye pikipiki nyingi… walivamia soko. Walifyatua risasi na kuuwa watu 21,” afisa mmoja wa serikali ya mtaa wa Madagali aliliambia AFP kuhusu shambulio la Jumanne jioni, kwa sharti la kutotajwa jina.

“Bado tunaendelea kutafuta miili zaidi kwani huenda baadhi walifariki porini kutokana na majeraha ya risasi walipokuwa wakijaribu kujinusuru.”

Soko laporwa

Wavamizi hao pia walipora soko na kuiba vyakula pamoja na pikipiki, chanzo hicho kilisema.

Watu wengine wanne, wakiwemo wanajeshi watatu, waliuawa katika mji jirani wa Hong, mkazi Ezekiel Musa aliliambia AFP.

“Boko Haram walitushambulia baada ya kuondoka mjini. Tuliona miili ya askari watatu na mwanamke mmoja pia aliuawa,” Musa alisema.

“Sasa mji una walinzi wa usalama lakini baadhi yetu tayari tumeanza kuondoka kwa hofu ya yaliyotokea.”

Gavana alaani shambulio

Gavana wa jimbo hilo, Adamu Umaru Fintiri, alilaani shambulio hilo bila kutoa idadi rasmi ya waliouawa katika taarifa yake.

“Hatutawaruhusu magaidi kudhoofisha juhudi zetu za kurejesha amani na utulivu,” alisema katika taarifa hiyo.

“Nawaonya wahusika: acheni mashambulizi haya yasiyo na maana au sivyo mkabiliane na nguvu kamili ya azma yetu ya pamoja.”

Tangu mwaka 2009, mashambulizi ya Boko Haram na magaidi wanaohusishwa na Islamic State (Daesh) yamesababisha zaidi ya watu 40,000 kuuawa na wengine milioni mbili kuyahama makazi yao katika eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Nigeria pia inakabiliana na makundi mengine yenye silaha ambayo yameongeza changamoto za usalama katika kaskazini mwa nchi hiyo.

CHANZO:AFP