Serikali ya Tanzania imeagiza mamlaka za nidhamu kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wa umma waliobainika kughushi barua za uhamisho na nyaraka nyingine za kiutumishi, ikisisitiza kuwa haitavumilia vitendo vinavyokiuka maadili na sheria za utumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ametoa maagizo hayo Juni 1, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa vitengo vya utumishi wa umma, akisema tayari baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Amesema vitendo hivyo vinachangia kudhoofisha ufanisi wa utendaji kazi na kuongeza malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za umma, huku akisisitiza matumizi ya TEHAMA kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Aidha, ameitaka serikali na waajiri kuhakikisha wanashughulikia kwa wakati mafao ya wastaafu ili kuepuka usumbufu usio wa lazima. Kwa upande wake, Katibu Mkuu Juma Mkomi amesema bado kuna changamoto ya ucheleweshaji wa huduma katika baadhi ya taasisi kutokana na kutofuata taratibu na miongozo ya kiutendaji.
Serikali imesema kikao hicho kinalenga kuimarisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


















