Umoja wa Mataifa umetenga Dola milioni 60 kama fungu la dharura la kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika eneo la Afrika ya Kati.
"Ni lazima tukabiliane na ugonjwa huu. Leo hii, ninatenga Dola milioni 60 kutoka Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa kuongeza kasi ya kukabiliana na janga la Ebola nchini DRC na sehemu nyinginezo," alisema Tom Fletcher Afisa Mwandamizi wa mfuo huo.
Kulingana na Fletcher, mchakato huo unaratibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus.
"Bado tunakumbana na changamoto kubwa kwenye epidemiolojia ya ugonjwa huu, wakati ambao bado hatujapata chanjo mahususi za kirusi cha Bundibugyo," aliongeza.
Ebola ni ugonjwa hatari unaosambazwa kwa kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.
Dalili zake ni pamoja na homa kali, kutapika, kuharisha, uchovu mkubwa na kutokwa damu.














