Joaquin “El Chapo” Guzman, kiongozi wa zamani wa genge la madawa wa kulevya nchini Mexico, ameiandikia barua mahakama ya New York, akiomba kurudishwa nchini Mexico kwa ajili ya kuendelea na kesi yake.
Guzman, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha katika gereza lenye ulinzi mkali huko Colorado, anadai kuwa, amekuwa akiteswa ndani ya gereza hilo.
“Nimeandika barua kadhaa nikiainisha haki ya rufaa yangu ya kusikilizwa kwa haki chini ya sheria. Hili ni ombi la heshima na naiomba mahakama hiyo ya wilaya, niweze kurudishwa nyumbani nikakabiliane na kesi yangu,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo, barua hiyo ilipingwa na Jaji wa mahakama hiyo, Brian M. Cogan, akisisitiza kuwa hoja za Guzman hazikuwa na mashiko yoyote ya kisiasa.
Kulingana na Jaji huyo, Guzman alimuandika barua tano, akiomba kupewa ahueni mablimbali, ikiwemo kuachiwa na kurudishwa nchini mwake.
Guzman anakumbukwa kwa kuongoza genge maarufu la Sinaloa huko Mexico, ambalo lilihusika kwa kiasi kikubwa na matukio ya kihalifu nchini humo.
Licha ya kufungwa gerezani, El Chapo bado alifanikiwa kutoroka jela mara mbili, kabla ya kukamatwa kwake mwaka 2016 na baadaye kuhamishiwa Marekani.












