Serikali ya Marekani imesema itahakikisha kuwa timu ya mpira wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaweza kusafiri na kushiriki katika michuano ya Kombe la Dunia, na kuilegezea masharti ya kuingia kufuatia marufuku ya Ebola.
"Tunatarajia timu ya DRC itaweza kushiriki Kombe la Dunia," afisa mmoja wa serikali ya Marekani amesema bila kutaka kutajwa jina lake.
Marekani imepiga marufuku raia wasio wa nchi yake ambao wamekuwa DRC, Uganda na Sudan Kusini katika kipindi cha siku 21 zilizopita kutokana na mlipuko hatari wa Ebola.
Afisa huyo wa Marekani amesema, timu ya DRC imekuwa ikifanya mazoezi Ulaya kwa hiyo haiusiani na masharti hayo.
Uchunguzi mkali
Lakini kama wangekuwa nchini DRC katika siku 21 zilizopita, wangetakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina kama ilivyo kwa raia wa Marekani wanaorudi-lakini sio marufuku ya moja kwa moja.















