Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Brian Mundubile amesema siku ya Jumatano kuwa ataelekea mahakamani kupinga matokeo ya wiki hii ya uchaguzi wa urais, akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika matokeo hayo ambayo Rais Hakainde Hichilema alichaguliwa tena kwa muhula wa pili.
"Watu wetu wamefuatilia matukio ya udanganyifu katika maeneo kadhaa, kutokuwepo kwa uwazi kuhusu mienendo, kuhesabiwa, kuwasilisha na kutangazwa kwa matokeo", Mundubile alisema katika taarifa.
Mpanga mikakati ya uchaguzi wa Hichilema hakutaka kuzungumza suala hilo kwa sasa lakini akasema kuwa atalizungumzia baadaye.
Tume ya uchaguzi ilimtangaza Hichilema mshindi akipata karibu 60% ya kura zilizopigwa, ikilinganishwa na 38% za Mundubile.
Uchaguzi uliokuwa na taharuki
Hali ilikuwa tete kuelekea uchaguzi wa Agosti 13 katika taifa hilo lenye utajiri wa madini la Kusini mwa Afrika lenye idadi ya watu milioni 22.
Mamlaka nchini Zambia ziliwakamata watu 11, ikiwemo viongozi waandamizi wa upinzani.
Tume ya uchaguzi ilisimamisha kuhesabu kura kwa saa kadhaa kutokana na taarifa za vurugu dhidi ya maafisa wa uchaguzi na wizi wa masanduku ya kura.


















