Zaidi ya Waisraeli nusu milioni waliondoka nchini na hawakurejea katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya vita vya Gaza, gazeti la Times of Israel liliripoti Jumapili, likinukuu Mamlaka ya Idadi ya Watu na Uhamiaji.
Takwimu za mamlaka hiyo zinaonyesha kuwa idadi ya Waisraeli walioondoka nchini tangu Oktoba mwaka jana ni karibu 550,000 - zaidi ya wale waliorejea Pasaka mwaka huu mwezi wa Aprili.
Tovuti ya habari ilisema kwamba kile ambacho kinaweza kuwa kutoroka kwa muda kwa Waisraeli wakati wa vita au shida za kiufundi za kurudi sasa kimegeuka kuwa mwelekeo wa kudumu au uhamiaji wa kudumu.
Kwa mujibu wa data kutoka Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israel, mwezi Aprili, idadi ya watu wa Israel ilifikia milioni 9.9, wakiwemo Wapalestina zaidi ya milioni 2, Wapalestina 400,000 katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na Wasyria 20,000 katika Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Mamilioni ya Waisraeli wana uraia wa nchi mbili kwani wanamiliki angalau utaifa mwingine mmoja pamoja na uraia wao wa Israel.
Vita vya Israel Gaza
Israel, ikikiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano, imekabiliwa na shutuma za kimataifa kutokana na kuendelea na mashambulizi ya kikatili huko Gaza tangu shambulio la Oktoba 7 mwaka jana na kundi la muqawama la Palestina Hamas.
Zaidi ya Wapalestina 37,500 wameuawa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na karibu wengine 86,000 wamejeruhiwa, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Zaidi ya miezi minane ya vita vya Israel, maeneo makubwa ya Gaza yapo kwenye magofu huku kukiwa na kizuizi cha chakula, maji safi na dawa.
Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo uamuzi wake wa hivi punde uliiamuru kusitisha mara moja operesheni yake katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni 1 walitafuta hifadhi kutokana na vita kabla ya kuvamiwa Mei 6.