Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer alisema Jumamosi kwamba atafutilia mbali mpango wenye utata wa kuwasafirisha maelfu ya waomba hifadhi kutoka Uingereza hadi Rwanda katika tangazo lake kuu la kwanza la sera tangu apate ushindi wa kishindo katika uchaguzi.
Serikali iliyopita ya kihafidhina ilitangaza mpango huo kwa mara ya kwanza mwaka 2022 wa kupeleka wahamiaji waliofika Uingereza bila kibali katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ikisema kuwa itakomesha waomba hifadhi wanaowasili kwa boti ndogo.
Lakini hakuna aliyetumwa Rwanda chini ya mpango huo kwa sababu ya miaka mingi ya changamoto za kisheria.
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu kuwa waziri mkuu, Starmer alisema kuwa sera ya Rwanda itafutiliwa mbali kwa sababu ni takriban 1% tu ya wanaotafuta hifadhi wangeondolewa na ingeshindwa kuwa kikwazo kwa wahamiaji zaidi.
Mpango umekufa na kusahaulika
"Mpango wa Rwanda ulikufa na kuzikwa kabla ya kuanza. Haijawahi kuwa kizuizi," Starmer alisema. "Siko tayari kuendelea na hatua ambazo hazifanyi kama kizuizi."
Starmer alishinda moja ya bunge kubwa zaidi katika historia ya kisasa ya Uingereza siku ya Ijumaa, na kumfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi wa Uingereza tangu Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair, lakini anakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za umma zinazotatizika na kufufua uchumi dhaifu.
Viongozi wa Afrika wamejitokeza kumpongeza Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.
''Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa pongezi zangu za dhati kwa Sir Keir Starmer kwa ushindi wa uchaguzi wa Chama cha Labour cha Uingereza na kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza,'' aliandika Rais Samia Suluhu katika mtandao wa X.
Tutaendelea kushirikiana
Rais Samia aliongeza kuwa anatarajia kuendelea kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza katika kutatua changamoto za kimataifa na kukuza maendeleo ya kiuchumi kwa watu wa nchi zetu mbili.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu alisifu "nia na ujasiri" wa Starmer katika miaka yake yote kwenye upinzani.
"Ninatarajia kuimarisha uhusiano kati ya Nigeria na Uingereza katika maeneo yenye maslahi na kuimarisha taasisi za kidemokrasia," alisema katika taarifa yake.
Rais wa Kenya William Ruto alisema ushindi wa Starmer ni "ushuhuda wa shauku kubwa ya raia wa Uingereza kwa siasa na sera zinazoendelea".
"Niko tayari kufanya kazi na Waziri Mkuu Starmer kukuza ushirikiano wetu wa kibiashara, kiulinzi na kisiasa huku tukichangia pamoja katika kujenga mustakabali ulio salama, wenye usawa na endelevu wa kimataifa," alisema kwenye chapisho kwenye X.
Katika taarifa yake, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema anatazamia kufanya kazi na Waziri Mkuu Starmer ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.