Israel iliapa "kuendeleza vita vyake" dhidi ya Hamas licha ya mapatano huko Gaza, kulingana na taarifa rasmi iliyotumwa kwa AFP na ofisi ya waziri mkuu.
"Serikali ya Israel, jeshi la Israel na vikosi vya usalama vitaendeleza vita vya kuwarudisha wote waliotekwa nyara, kuwaondoa Hamas na kuhakikisha kuwa hakuna tena tishio lolote kwa serikali ya Israel kutoka Gaza," taarifa hiyo ilisema mapema Jumatano.
AFP inaripoti kuwa kabla ya upigaji kura wa baraza la mawaziri, Netanyahu alikabiliwa na uasi kutoka ndani ya muungano wake wa mrengo wa kulia, ambao baadhi yao wanaamini kuwa uliwaridhia mengi kupita kiasi Wapalestina ambao wameapa kuwaponda.
Waziri Mkali wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir aliashiria kuwa atapiga kura dhidi ya makubaliano hayo, akisema ni lazima kujumuisha kuachiliwa kwa wanajeshi wa Israel pia waliochukuliwa na Hamas.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema kabla ya mkutano huo muhimu kuwa amepata hakikisho kwamba makubaliano hayo hayatamaanisha mwisho wa vita vya kuiangamiza Hamas.
"Mara tu baada ya kumaliza awamu hii", alisema, operesheni za usalama "zitaendelea kwa nguvu zote."
Rais wa Marekani Joe Biden alisema amefarijika sana kwamba baadhi ya mateka wataachiliwa hivi karibuni chini ya makubaliano yaliyoandaliwa kwa msaada kutoka Mashariki ya Kati.
"Nimefurahia sana kwamba baadhi ya watu hawa wajasiri wataunganishwa tena na familia zao mara tu mpango huu utakapotekelezwa kikamilifu," Biden alisema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani.
Urusi pia ilikaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano ya kibinadamu kati ya Israel na Hamas, shirika la habari la RIA limemnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova.
'Vita itaendelea'
Katika taarifa yake, serikali ya Israel imesisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayatamaanisha mwisho wa vita huko Gaza.
Israel "itaendeleza vita ili kuwarejesha nyumbani mateka wote, kukamilisha kuondolewa kwa Hamas na kuhakikisha kuwa hakutakuwa na tishio jipya kwa Jimbo la Israel kutoka Gaza," taarifa ya serikali ilisema.
Takriban Wapalestina 14,128, idadi kubwa ya raia, wameuawa Gaza tangu mashambulizi ya anga ya Israel yaanze baada ya Oktoba 7, kulingana na serikali katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Sasisho la hivi punde la idadi ya vifo linajumuisha angalau watoto 5,600 na wanawake 3,550.