Iran itafanya marudio ya uchaguzi wa rais kuchukua nafasi ya marehemu Rais Ebrahim Raisi, afisa mmoja amesema baada ya kura ya awali kuona wagombea wakuu hawakupata ushindi wa moja kwa moja.
Uchaguzi wa marudio wa Julai 5 sasa utawakutanisha Masoud Pezeshkian na msuluhishi wa zamani wa nyuklia Saeed Jalili.
Mohsen Eslami, msemaji wa uchaguzi, alitangaza matokeo hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na televisheni ya taifa ya Iran siku ya Jumamosi. Alisema kati ya kura milioni 24.5 zilizopigwa, Pezeshkian alipata milioni 10.4 huku Jalili akipata milioni 9.4. Spika wa Bunge Mohammad Bagher Qalibaf alipata milioni 3.3. Mostafa Pourmohammadi alikuwa na zaidi ya kura 206,000.
Uchaguzi wa haraka wa Iran ulifanyika baada ya marehemu Rais Ebrahim Raisi kuuawa katika ajali ya helikopta mwezi uliopita.
Matokeo ya awali yalikuja baada ya uchaguzi wa 14 wa rais nchini Iran kukamilika baada ya shughuli ya upigaji kura iliyochukua saa 18.
Msemaji wa makao makuu ya uchaguzi ya Iran, Mohsen Eslami, alisema mchakato huo ulikamilika usiku wa manane kwa saa za huko.
Kuunda mazingira ya kisiasa ya Iran
Lakini Wizara ya Mambo ya Ndani, ambayo inasimamia uchaguzi huo, ilirefusha upigaji kura mara tatu ili kuruhusu wapiga kura wengi zaidi kupiga kura.
Wagombea wanne - Mohammad Baqer Qalibaf, Jalili, Pezeshkian na Mostafa Pourmohammadi - wanawania kiti cha urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia kifo cha rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta mwezi uliopita.
Takriban wapiga kura milioni 64 nchini Iran walistahili kupiga kura katika uchaguzi huo, wengi wao wakiwa ni vijana. Katika uchaguzi wa urais wa 2021, milioni 59.3 walistahiki kupiga kura.
Jumla ya vituo 58,640 vya kupigia kura viliundwa kote nchini ili kuwezesha mchakato wa upigaji kura, zaidi ya 6,000 kati yao vikiwa Tehran.
Nje ya nchi, Wizara ya Mambo ya Nje iliteua vituo 344 vya kupigia kura vya ng'ambo kwa ajili ya Wairani kutekeleza haki yao, isipokuwa Kanada, ambayo haikuruhusu.
Uchaguzi wa 2021, wakati Raisi alishinda kwa kishindo, ulishuhudia idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kufikia asilimia 49.
Matokeo ya uchaguzi huu muhimu yanasubiriwa kwa hamu kwani yanaweza kuchagiza pakubwa hali ya kisiasa ya Iran kusonga mbele.