Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani ambae anakabiliwa na mashtaka 34. 

Jopo la waamuzi la mji wa New York limemhukumu Donald Trump kwa mashtaka yote katika kesi yake ya kulipa pesa za kunyamazisha Alhamisi, tukio kubwa ambalo limekuja miezi mitano kabla ya uchaguzi ambapo anataka kurudi White House kama rais.

Kesi ya kwanza ya kihistoria ya jinai ya rais wa zamani wa Marekani ilimalizika na Trump mwenye umri wa miaka 77 kukutwa na hatia kwa kila moja ya mashtaka 34 ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo yaliyokusudiwa kumnyamazisha mwigizaji wa filamu ya watu wazima, Stormy Daniels.

Trump hakujibu mara moja lakini alikaa kimya, mabega yake yakining’inia.

Hukumu hiyo inaitumbukiza Marekani katika eneo la kisiasa lisilojulikana lakini haimzuii Trump kugombea tena.

Majadiliano kwa zaidi ya saa 11

Uamuzi huo unakuja wiki chache kabla ya Mkutano wa Kitaifa wa Republican huko mji wa Milwaukee, ambapo Trump anatarajiwa kupokea uteuzi rasmi wa chama hicho kupambana na Rais Joe Biden mnamo Novemba 5.

Jopo la waamuzi 12 lilijadili kwa zaidi ya saa 11 kwa siku mbili mwishoni mwa kesi ya wiki tano iliyofanyika katika mahakama ya Manhattan.

Trump alihukumiwa kwa kughushi rekodi za biashara ili kumlipa wakili wake, Michael Cohen, kwa malipo ya $130,000 kwa Stormy Daniels siku moja kabla ya uchaguzi wa 2016, wakati madai yake yangekuwa na athari mbaya kisiasa kwa Trump.

Kesi hiyo ilijumuisha ushuhuda mrefu kutoka kwa mwigizaji huyo wa filamu, ambaye jina lake halisi ni Stephanie Clifford na alielezea kwa kina mahakamani kile kilichotokea walivyokutana kimwili na Trump mwaka 2006.

Donald Trump

Trump alikuwa na mawazo wakati wa kesi

Waendesha mashtaka walifanikiwa kueleza kesi yao wakidai kwamba pesa za kunyamazisha na kuficha malipo hayo zilikuwa sehemu ya uhalifu mkubwa wa kuzuia wapiga kura kujua kuhusu tabia ya Trump.

Mawakili wa utetezi wa Trump walijibu kwamba "kujaribu kuathiri uchaguzi" ilikuwa ni "demokrasia" tu na kwamba rais wa zamani hakufanya kosa lolote.

Kesi hiyo imeingiliana na mipango ya Trump wa kushindana na Rais Biden.

Hata hivyo, alitumia fursa hiyo ya vyombo vya habari kila siku, akitoa hotuba mbele ya kamera nje ya mahakama akilalamika kuwa muathirika wa kisiasa.

Waamuzi wasiojulikana

Utambulisho wa waamuzi 12 walioamua kesi hiyo ulikuwa siri, utaratibu adimu zaidi unaoonekana katika kesi zinazohusisha mafia au watuhumiwa wengine wa vurugu.

Baada ya kushawishi uwezekano kwa wiki kadhaa, Trump - ambaye alikanusha kuwa na ukaribu wowote na Daniels katika shindano la gofu la 2006 - aliamua kutojitetea.

Mwana Republican huyo, ambaye alijulikana kama mjasiriamali mkubwa wa mali isiyohamishika kabla ya kupanda ghafla hadi nafasi ya juu kabisa nchini katika uchaguzi wa 2016, sasa anakabiliwa na kifungo cha gerezani au, zaidi, uangalizi wa kifungo cha nje.

Kwa nadharia, anaweza kukabiliwa na hadi miaka minne gerezani kwa kila kosa la kughushi rekodi za biashara lakini wataalamu wa sheria walisema kama mhalifu wa mara ya kwanza ni vigumu kwenda gerezani.

Rufaa

Rufaa inaweza kuchukua miezi kadhaa kukamilika.

Iwapo atashinda urais, hataweza kujisamehe, kwa kuwa kesi hiyo haikuletwa na serikali ya shirikisho bali na serikali ya New York, ambapo ni gavana pekee anayeweza kumsafisha jina.

Trump pia anakabiliwa na mashtaka ya shirikisho na serikali ya kula njama ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020 ulioshindwa na Biden, na kwa kuhifadhi nyaraka za siri baada ya kuondoka Ikulu.

AFP