Picha za video zikimuonesha kiongozi huyo ndani ya helikopta hiyo./Picha:Wengine  

Helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran, Ebrahim Raisi na maofisa wengine 'ilipata matatizo' wakati wa kutua katika eneo la jimbo la Kaskazini Magharibi mwa Azerbaijan , siku ya Jumapili, kulingana na kituo cha televisheni cha taila la Iran.

Raisi alikuwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, Gavana wa Azerbaijan Mashariki, Malik Rehmati na kiongozi wa sala ya ijumaa katika mji wa Tabriz Al-Hashem, wakati wa tukio hilo.

Vyombo vya habari vya taifa hilo vinasema kuwa vikosi vya uokoaji vipatavyo 20 kutoka majimbo ya Mashariki ya Azerbaijan, Ardabil na Zanjan viko katika eneo hilo kusaidia shughuli za uokoaji.

Hadi sasa, hakuna ripoti kuhusu hali ya waliokuwemo kwenye helikopta hiyo, akiwemo Raisi. Shughuli ya uokoaji inaweza kuchukua saa kadhaa kutokana na eneo hilo la milimani kuwa na ukungu mzito.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi aliambia runinga ya serikali kwamba ujumbe unaoongozwa na Raisi ulikuwa unarejea kutoka kwenye sherehe ya uzinduzi wa bwawa kwenye mpaka wa Azerbaijan na Iran wakati tukio hilo lilipotokea.

Alisema moja ya helikopta katika msafara wa rais wa Iran "ilitua kwa shida" kutokana na hali mbaya ya hewa, na kuongeza kuwa timu nyingi za uokoaji zimetakiwa kuchukua hatua.

Pir Hossein Kolivand, kiongozi wa kituo cha Red Crescent, amekiambia kituo cha taifa cha televisheni cha nchi hiyo kuwa vikosi 40 vya uokoaji vimepelekwa katika eneo hilo.

Vikosi hivyo ni kutoka miji ya Tehran, Alborz, Ardabil, Zanjan eneo la mashariki na kaskazini mwa Azerbaijan, wakiwemo wale wenye uzoefu na utalaamu mkubwa, alisema.

Pia wamo mbwa 15 wa kunusa pamoja na ndege mbili zisizo na rubani.

Kutokana na hali mbaya ya hewa na ukungu mkubwa katika mkoa huo, kwa sasa haiwezekani kuruka helikopta za uokoaji, alisema.

Ali Bahadori Jahromi, msemaji wa serikali, katika chapisho kwenye mtandao wa X alisema mkutano wa Baraza la Mawaziri la serikali ulifanyika Jumapili na tukio la Azabajani Mashariki lilijadiliwa.

Mohammad Mokhber, makamu wa kwanza wa rais, ambaye aliongoza mkutano huo mara moja aliondoka kuelekea mji wa kaskazini wa Tabriz pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali wenye hadhi ya juu, Jahromi alisema.

Tukio hilo limetokea baada ya Raisi kuungana na mwenzake wa Kiazabajani Ilham Aliyev kwa ajili ya uzinduzi na wa mitambo ya maji katika mpaka na Azerbaijan.

Viongozi wa nchi hizo mbili walifanya mazungumzo ya pande mbili, ambayo yalifuatiwa na sherehe ya uzinduzi wa "Khudaferin" na "Qiz Qalasi" kwenye Mto Araz.

Wakati huo huo, Televisheni ya taifa ilionyesha picha za watu eneo la Imam Reza katika mji aliozaliwa Raisi Mashhad wakimuombea rais na wengine waliokuwa kwenye helikopta hiyo.

Raisi hapo awali aliongoza madhabahu ya Mashhad kabla ya kuwa afisa mkuu wa mahakama ya nchi hiyo na baadaye, alichukua usukani wa serikali mnamo 2021 na ushindi wa kishindo katika uchaguzi.

Hali ya hewa kutatiza uokoaji

Waokoaji walikuwa wakijaribu kufikia eneo hilo, TV ya serikali ilisema hapo awali, lakini walikuwa wametatizwa na hali mbaya ya hewa. Kulikuwa na mvua kubwa na ukungu ulioripotiwa na upepo fulani. IRNA ililielezea eneo hilo kama "msitu" na lenye milima mingi.

Raisi alikuwa Azerbaijan mapema Jumapili kuzindua bwawa na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev. Bwawa hilo ni la tatu ambalo mataifa hayo mawili yalijenga kwenye Mto Aras. Ziara hiyo ilikuja licha ya uhusiano mbaya kati ya mataifa hayo mawili, ikiwa ni pamoja na shambulio la bunduki kwenye Ubalozi wa Azerbaijan mjini Tehran mwaka 2023, na uhusiano wa kidiplomasia wa Azerbaijan na Israeli, ambao demokrasia ya Kishia ya Iran inauona kama adui yake mkuu katika eneo hilo.

Iran ina huduma mbalimbali za helikopta nchini humo, lakini vikwazo vya kimataifa vinafanya iwe vigumu kupata sehemu za ndege hizo. Meli zake za anga za kijeshi pia zilianzia kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.

Raisi, 63, aliongoza mahakama ya zamani nchini humo. Anaonekana kama mfuasi wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei na baadhi ya wachambuzi wamependekeza kuwa anaweza kuchukua nafasi ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 85 baada ya kifo chake au kujiuzulu kutoka kwa wadhifa huo.

Raisi alishinda uchaguzi wa rais wa Iran wa 2021, kura ambayo ilishuhudia idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura katika historia ya nchi hiyo. Raisi amewekewa vikwazo na Marekani kwa sehemu kutokana na kuhusika kwake katika mauaji makubwa ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa mwaka 1988 mwishoni mwa vita vya umwagaji damu vya Iran na Iraq.

Chini ya Raisi, Iran sasa inarutubisha uranium katika viwango vya karibu vya kiwango cha silaha na kutatiza ukaguzi wa kimataifa.

TRT Afrika